MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) imeandaa tamasha kubwa la kuadhimisha miaka kumi (10) kutoka uanzishwe mwaka 2004 kwa michezo mbalimbali ukiwemo mpambano wa maveterani wa watani wa jadi Simba na Yanga litakalofanyika kilele cha sherehe hizo uwanja wa Karume,Dar es Salaam Desemba 25,(Krismasi) mwaka huu.
Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib alisema katika wiki ya maadhimisho hayo, Desemba 24 sherehe hizo zitatanguliwa na ugawaji wa nyumba 38 zilizojengwa na wanachama wa SHIWATA kwa njia ya kuchangiana na kufikisha idadi ya jumla ya nyumba 104 ambazo mpaka sasa zimekwisha jengwa katika kijiji cha wasanii Mwanzega, Mkuranga chenye ekari 300 kwa ajili ya makazi.
Alisema ili kuwavutia wenye nyumba hizo wahamie kijijini, SHIWATA imetoa eneo maalumu kwa ajili ya kulima bustani ya mboga mboga na mazao ambayo si ya kudumu ili wajikimu wao wenyewe na familia zinazowazunguka.
Alisema SHIWATA unaomiliki shamba la ekari 500 katika kijiji cha Ngarambe, Mkuranga unasimamia usafishaji wa shamba hilo kutumia mtambo wa kisasa (bulldozer) lililokodishwa kutoka Kampuni ya Willy Enterprises Ltd ya Dar es Salaam kwa gharama ya sh. mil. 22 kwa siku 20 kukamilisha kazi hiyo.
Alisema Bulldozer hilo limefikisha siku kumi sasa kutoka kazi ya kusafisha shamba hilo na kung’oa visiki ianze, wanachama 90 waliomilikishwa sehemu ya shamba kwa lengo la kulima mazao yanayostawi eneo hilo, wameanza kuchangia gharama za kusafisha shamba hilo.
Mwenyekiti huyo alisema mazao yanayostawi eneo hilo ni mpunga, mahindi, mbaazi, viazi vitamu, ndizi, kunde, korosho, mtama na matunda kama embe, machungwa, matikiti maji na mafenesi.
Alisema pia kuwa sherehe za maadhimisho hayo zitawakutanisha wakongwe wa soka wa Simba na Yanga ambao ni wanachama wa SHIWATA wamekubali kushiriki mpambano huo.
Kwa upande wa Yanga, mchezaji wa zamani wa Klabu hiyo, Mtwa Kiwhelo na Athumani Juma Chama kwa upande wa Simba wanawawakilisha wenzao katika maandalizi ya awali ya mchezo huo.
SHIWATA yenye wanachama zaidi ya 8,000 kutoka fani mbalimbali za sanaa za maigizo, mpira wa miguu, mpira wa wavu, netiboli, waigizai wa filamu, muziki wa dansi, muziki wa kizazi kipya, vijana na waandishi wa Habari kila kundi litapewa nafasi ya kuonesha vipaji vyao siku hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...