Na John Gagarini, Bagamoyo
SUALA la Maabara kwa shule za Sekondari za Kata limeingia kwenye hatua
nzito baada ya mkuu wa Mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza kuiacha ofisi yake na
kuhamia Wilaya ya Bagamoyo ili kuhakikisha agizo la Rais Dk Jakaya Kikwete
la kila wilaya iwe imekamilisha ujenzi huo ifikapo Novemba 30 mwaka huu.
Sambamba na hilo mkuu huyo amewataka wakuu wa idara wa Wilaya hiyo kila
mmoja kutokaa ofisini na kuchagua kata ya kwenda ili kusimamia ujenzi huo
hadi ujenzi wa maabara ukamilike.
Akizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika mjini
Bagamoyo Mahiza alisema kuwa ujenzi wa maabara kwenye wilaya hiyo bado
zoezi hilo haliko vizuri hivyo lazima itumike nguvu ya ziada kufanikisha
zoezi hilo.
“Kuanzia sasa najua nitaanzia kata gani lakini nahamia Bagamoyo na wakuu wa
idara kila mmoja tukitoka hapa ataniambia atakuwa kata gani ili tuanze
usimamizi kwani bila ya kufanya hivi muda utaisha na mambo yatakuwa
magumu,” alisema Mahiza.
“Kuanzia sasa vikao vya madiwani havitakuwepo kilichobaki wote tuende
kwenye ujenzi wa maabara na kama mtu anaona hawezi kuwajibika aondoke
mapema asije akatuharibia mipango yetu ya maendeleo kwani watoto ni wetu,”
alisema Mahiza.
Mahiza alisema kuanzia sasa hivi hakuna cha mahafali wala sherehe wimbo
uliopo ni maabara kwa shule zetu za sekondari kwani baadhi ndo wako kwenye
msingi je ujenzi utakamilika kwa wakati jambo ambalo linatia mashaka.
“Baadhi ya watendaji hawana haraka na kusababisha shughuli kwenda taratibu
kuanzia sasa hapa ni mwendo wa kufanya kazi kwani tusipokuwa makini muda
utaisha hatujakamilisha itakuwa haipendezi,” alisema Mahiza.
Aidha alisema kuwa wakuu wa wilaya na mikoa waliitwa Dodoma na Rais na
kutakiwa wawe wamekamilisha ujenzi huo ifikapo Novemba 30 mwaka huu na wao
walimwahidi kuwa watakamilisha ujenzi kipindi hicho.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo Shukuru Mbato alisema
kuwa agizo hilo wamelipokea na watahakikisha wanakamilisha ujenzi wa
maabara hizo kwa muda uliopangwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...