Na Saidi Mkabakuli, Sumbawanga

Serikali imeazimia kuanza kuiboresha bandari ya kimkakati ya Kasanga inayohudumia nchi za Burundi, Rwanda na Kongo iliyopo katika Ziwa Tanganyika, mkoani Rukwa.

Ahadi hiyo imetolewa na Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya miundombinu katika Bandari ya Kasanga.

Bibi Mwanri alisema kuwa serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania imepanga kuboresha bandari zote ili kuwa malango kuu la biashara kwa soko la ndani na kwa nchi jirani ili kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena kwa ufanisi.

“Tumedhamiria kuendelea kuboresha miundombinu ya bandari hususan miradi iliyoibuliwa katika Programu ya Matokeo Makubwa Sasa ikiwemo Bandari ya Kasanga ili kuweza kukidhi mahitaji ya utoaji wa huduma katika eneo hili,” alisema.

Bibi Mwanri aliongeza kuwa serikali pia imejipanga kuendelea kuboresha miundombinu na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kuhudumia shehena katika bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Kasanga na Kigoma na kukamilisha maandalizi ya ujenzi wa bandari mpya za Mwambani (Tanga), Mbegani (Bagamoyo) na Bandari Kavu ya Kisarawe.

Akizungumza na ugeni huo, Msimamizi Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa alisema kuwa Bandari hiyo ina fursa nyingi katika kuhudumia shehena na abiria wanaopitia bandarini hapo.

“Bandari yetu ina fursa kubwa za kibiashara kwani tuna wateja wengi kutoka ndani na nje ya nchi wanaotumia bandari yetu kupitishia bidhaa zao, pamoja na abiria wanaosafiri kwenda nje na ndani ya Tanzania,” alisema.

Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka ujao wa fedha Serikali imedhamiria kuboresha mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kuwekeza katika kujenga miuondombinu na kuboresha usafirishaji wa mizigo katika bandari zote nchini.

Pia, Mpango huo unaweka bayana kuendeleza na ukarabati na ununuzi wa vyombo vya usafiri na usafirishaji katika maziwa.
Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Watatu kushoto) akimsikiliza kwa makini Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kulia) mara walipowasili katika bandari hiyo kujionea shughuli mbalimbali za maendeleo bandari hapo.
Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kushoto) akiwaongoza wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kujionea moja ya meli za kigeni zinazotia nanga katika bandari hiyo. Meli hiyo ni MV Rwegura kutoka nchini Burundi.
Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kushoto) akiongea na wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kuhusu namna ya kuhudumia meli kutoka nje ya nchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...