Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimtunuku shahada ya PhD ya Sayansi Uhandisi na Hesabu Bw. Jonas Petro Senzige kwenye Mahafali ya pili ya Taasisi hiyo iliyofanyika leo jijini Arusha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia kwenye Mahafali ya 2 ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyofanyika leo jijini Arusha.
Sehemu ya wahitimu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela
Wahahitimu w PhD katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela
Wahahitimu w PhD katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanmzania ambae pia ni Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika maandamano na viongozi wa Taasisi hiyo pamoja na wahitimu, wakati wa Mahafali ya 2 ya Taasisi hiyo yaliyofanyika leo jijini Arusha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal na wakiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa Shahada ya Uzamili na Uzamifu kwenye Mahafali ya 2 ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyofanyika leo jijini Arusha.
Picha na OMR
HOTUBA YA
MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
AKIPOKEA SHAHADA YA HESHIMA YA UZAMIVU (HONORIS CAUSA) YA CHUO KIKUU CHA NELSON
MANDELA CHA SAYANSI NA TEKNOLOJIA, TAREHE 18 DESEMBA, 2014, ARUSHA
Shukrani
kwa Kutunukiwa Shahada
Mheshimiwa Dkt. Gharib Mohamed Bilal, Makamu wa
Rais na Mkuu wa Chuo;
Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa
Sayansi na Teknolojia; Mheshimiwa Profesa David Homeli Mwakyusa, Mwenyekiti wa
Baraza la Chuo;
Profesa Burton Mwamila; Makamu Mkuu wa Chuo;
Mheshimiwa Gatechew Engida, Naibu Mkurugenzi Mkuu
wa UNESCO;
Mheshimiwa Daudi Felix Tibenda; Mkuu wa Mkoa wa
Arusha;
Wanajumuia wote wa Chuo;
Wahitimu;
Mabibi na Mabwana.
Nasimama mbele yenu
kwa unyenyekevu mkubwa kupokea Shahada ya Heshima ya Uzamivu (Honoris Causa)
mliyonitunuku leo hii. Nashukuru kwa maneno mazuri yaliyosemwa juu yangu wakati
wa kunitunuku Shahada hii. Kutunukiwa kwa shahada hii ni heshima kubwa kwangu
na Watanzania wote. Heshima hii mliyonipa ni deni kubwa kwangu na kwa Serikali yetu
kuendelea kutimiza azma yake ya kutekeleza mapinduzi ya sayansi na teknolojia katika
sekta zote. Kwa kufanya hivyo,
tutatimiza matarajio yenu na kulinda hadhi na heshima ya Shahada hii. Nasi
hatutarudi nyuma na tutajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kufikia lengo hilo
jema.
Wakati nakubali
Shahada hii natambua mchango mkubwa wa wana-sayansi, wanawake na wanaume Watanzania
ambao juhudi zao zimetuwezesha kupiga hatua hii ya kuridhisha ya matumizi ya
sayansi na teknolojia. Napokea heshima hii na kuitoa kwa Watanzania wote ambao
mchango wao umewezesha nchi yetu kupiga hatua ya kutia moyo katika kuendeleza
sayansi na teknolojia.
Pongezi
kwa Uongozi wa Chuo
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Wanajumuia wote wa Chuo;
Niruhusu nikupongeze
wewe, Mkuu wa Chuo, na uongozi mzima wa Chuo chetu hiki muhimu kwa mafanikio
makubwa mliyoyapata katika kipindi kifupi cha uhai wake. Haya ni mahafali ya
pili tokea Chuo hiki kianzishwe, Inatia moyo kuona chini ya uongozi wenu Chuo
kinapata mafanikio makubwa. Idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka wanafunzi 44 wa shahada ya uzamili mwaka jana
hadi 91 mwaka huu. Hali kadhalika
idadi ya wanaohitimu kwa wakati nayo imeongezeka kutoka asilimia 83 hadi asilimia 93.
Nawapongeza sana wanafunzi na wahadhiri wa Chuo hiki walioshinda tuzo za
kimataifa zinazotolewa na Bill and Belinda Gates Foundation, Shirika la Chakula
Duniani (FAO) na Royal Academic of Engineering. Ushindi wenu ni ushahidi tosha wa
ubora wa Chuo chenyewe. Ndio maana pia kunakuweko na muitikio wa mashirika ya
ndani na ya kimataifa yanayojitokeza kufadhili wanafunzi wanaosoma katika Chuo
hiki na kufadhili programu za Chuo hiki. Nawaomba muendelee kushirikiana na
wadau wengine wa ndani na nje ili kuongeza wigo wa wadau kutoka vyuo vya
kimataifa mnavyoshirikiana navyo sasa.
Chuo hiki ni sehemu
ya mtandao wa vyuo vya Nelson Mandela vya Sayansi na Teknolojia katika Bara la
Afrika. Chuo hiki cha Arusha ni mahsusi kwa ajili ya kanda ya Afrika Mashariki.
Ndiyo maana Hati Idhini (University Charter) niliyokipa Chuo hiki inaeleza
bayana kuwa Chuo hiki kinapaswa kuwa chenye hadhi maalum (special status).
Hadhi hii yapaswa pia ionekane katika ubora wa elimu inayotolewa hapa. Aghalabu jambo hilo ni matokeo ya ubora wa wahadhiri
wake, programu zake na miundombinu yake. Nimesikia changamoto zinazowakabili
katika kufikia lengo hilo. Makamu Mkuu wa Chuo amezungumzia mahitaji ya
miundombinu na fedha kwa ajili ya uendeshaji na ufadhili wa wanafunzi. Napenda
kuwahakikishieni kuwa serikali inayo dhamira ya dhati ya kutatua changamoto
hizi na kwamba tutafanya kila tuwezalo tuwe wa msaada.
Wakati nilipokuwa nazindua
Chuo hiki, nilizindua pia Mfuko Maalum wa Dhamana wa Chuo yaani Endowment
Fund for Excellence. Niliahidi kuuchangia na leo natangaza kuwa Serikali
itatoa shilingi milioni 200 za
kuanzia na tutaendelea kuchangia
mara kwa mara. Nimefarijika kuona nanyi mmeanza kufanya juhudi za kuanzisha
mpango wa ubia na sekta binafsi wa Nelson Mandela Public Private Partnership
(NM-PPP). Huu ni uamuzi sahihi kabisa kwani kuhusisha sekta binafsi katika
uendelezaji wa Chuo hiki ni jambo la manufaa makubwa.
Umuhimu
wa Sayansi na Teknolojia Katika Kufanikisha
Dira
ya Taifa 2025
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Ni utamaduni
uliozoeleka na kukubalika kwa muda mrefu kuwa Mtunukiwa wa Shahada ya Heshima
ya Uzamivu hupewa fursa ya kutoa nasaha zake. Imekuwa ni kama wajibu
unaombatana na haki ya kupata Shahada yenyewe kiasi kwamba kukubali kimoja
yakupasa ukubali na kingine. Madhali nimekubali Shahada hii ya heshima,
nawajibika na sina budi kupokea heshima hii kwa kuzungumza. Mimi sio mwanasayansi
kitaaluma, lakini ni muumini na mshabiki mkubwa wa maendeleo ya sayansi na
teknolojia. Ni muumini wa dhati wa dhana kuwa, bila ya kuendeleza sayansi na
teknolojia, hakuna mapinduzi endelevu ya kimaendeleo. Hivyo basi kuendeleza
Mapinduzi ya sayansi na teknolojia si suala la hiyari, bali ni la lazima kwa
jamii yoyote ile inayotaka kujiletea maendeleo endelevu, kuondokana na
umasikini na kuzishinda changamoto zake.
Jamii
zote zilizopiga hatua kubwa za maendeleo zimefanya hivyo kwa kuwekeza katika sayansi
na teknolojia. Tanzania siyo kisiwa cha upweke.
Tunatambua kuwa hakuna maendeleo bila kuwekeza kwenye sayansi na
teknolojia. Dira ya Taifa ya Mwaka 2025
imetamka bayana kuwa Tanzania inalenga kuwa nchi ya uchumi wa kati, ifikapo
mwaka 2025. Ili kufikia kwenye lengo hilo adhimu kunahitajika mapinduzi katika uzalishaji,
hususan kilimo na viwanda, mapinduzi katika utoaji wa huduma na mapinduzi
katika uendelezaji wa rasilimali watu. Kichocheo cha mapinduzi hayo kufanyika
si kingine bali ni maendeleo na matumizi
ya sayansi na teknolojia.
Uhusiano wa Sayansi,
Teknolojia na Maendeleo
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Historia
imetufundisha kuwa nchi zilizoendelea zilianza na mapinduzi ya kilimo, kisha
mapinduzi ya viwanda na hatimaye mapinduzi ya huduma. Kichocheo kikubwa cha
mapinduzi hayo ilikuwa ni mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Hivyo ndivyo ilivyofanyika kwa wenzetu wengine
walioendelea, nasi hatuna budi kufuata mkondo huo. Wenzetu hao waliopiga hatua
kubwa sasa wameanza safari ya kujenga uchumi unaotegemea sio viwanda (industrial economy) pekee, bali ujuzi (knowledge based economy). Uchumi huu
unasukumwa zaidi sasa na ujuzi na ugunduzi (knowledge
and innovation) sio tena na uzalishaji (production)
pekee. Wameelekeza sasa tafiti zao kutafuta majawabu si tu ya sasa bali na hata
yale ya wakati ujao. Wanafikiria na kutafiti juu ya maisha katika sayari
nyingine nje ya dunia tunayoishi. Huko ndiko dunia inakoelekea, sisi hatuwezi kufanya
kinyume chake. Hatuwezi kubaki nyuma.
Jawabu pekee ni kuwekeza katika maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kuwa na chuo kama hiki ni uamuzi na hatua
sahihi.
Ripoti ya Ugunduzi
Duniani ya 2014 (Global Innovation Index) yenye kuhusisha nchi 143 zilizopimwa
kwa vigezo vinane, imezitaja nchi za Usiswi, Uingereza, Sweden, Finland, Uholanzi,
Marekani, Singapore, Denmark, Luxemburg na China (Hongkong) kuwa ni nchi
zinazoongoza kwa ugunduzi duniani. Tanzania inatajwa kuwa ni nchi ya 123 na nchi ya 24 kati ya 33 za Afrika.
Ripoti inazitaja, nchi 25
zinazoongoza kwa ugunduzi duniani kuwa ni nchi za uchumi wa kipato cha juu
(high income). Nchi za kipato cha kati na chini hazimo katika kundi hilo
kutokana na uwekezaji mdogo katika sayansi na teknolojia. Ukweli huu
unadhihirishwa zaidi na ripoti ya Global Research and Development Funding Forecast
ya 2014 inayoonyesha kuwa katika mwaka 2014, Marekani imepanga kutumia Dola Billioni 465 (asilimia 2.8 ya Pato
la Taifa), China Dola bilioni 284 (asilimia
2 ya pato la Taifa) na Japan Dola
bilioni 165 (asilimia 3.4 ya pato la Taifa) kwa ajili ya shughuli za
utafiti.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Takwimu nilizozitoa
zinaonyesha, pasipo na chembe ya shaka, kuwa uko uhusiano mkubwa kati ya
matumizi ya rasilimali katika sayansi na maendeleo makubwa. Somo tunalolipata
hapa ni kwamba hakuna mazingaombwe wala njia ya mkato ya kujipatia maendeleo ya
juu. Hatuna budi kuwekeza katika kuendeleza
sayansi na teknolojia nchini kama tunataka kutoka hapa tulipo. Hatuna budi
kuwekeza zaidi kwenye kufundisha
wanasayansi, na katika tafiti na ujenzi wa miundombinu ya kuwezesha wanasayansi
kufanya tafiti zao. Kwa muda mrefu sana
hili ni eneo ambalo hatukulipa uzito unaostahili. Tumefundisha na kuwekeza sana
katika kuwaandaa vijana wetu katika fani za sayansi za jamii, uongozi, siasa,
sheria na biashara. Pamoja na kada hizo kuwa muhimu, lakini wanasayansi ni
muhimu zaidi.
Hatua
za Serikali
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Mimi na Serikali
ninayoiongoza tumechukua hatua kadhaa kurekebisha kasoro hizi za kihistoria.
Wakati naingia madarakani, nimekuta hali katika eneo hili la sayansi na
teknolojia ikihitaji msukumo wa pekee. Idadi ya wanafunzi wa sayansi ilikuwa
ndogo na wanafunzi wengi hawakupenda kusoma masomo hayo maana hapakuwa na mazingira
ya kuvutia kusoma masomo ya sayansi shuleni na ya kimaisha kwa wale waliohitimu
masomo ya sayansi. Hapakuwa na ufadhili wa masomo ya sayansi hivyo ilikuwa pia
vigumu kwao kujiendeleza. Walimu wa sayansi nao walikuwa wachache, maabara za
sayansi katika shule zetu zilikuwa haba na katika shule nyingine zilikuwa
zimechakaa. Vituo vya utafiti vingi
vilikuwa vina miundombinu iliyoharibika na ajira za watafiti zilikuwa
zimesitishwa. Hapakuwa na fedha zinazotengwa mahsusi kwa ajili ya utafiti. Hali
kadhalika gharama za matumizi ya simu na intaneti nazo zilikuwa juu sana.
Tumefanya maamuzi
ambayo wakati mwingine yamestaajabisha wengi. Tumepanua udahili wa wanafunzi wa
masomo ya Sayansi kutoka wanafunzi 32,899
mwaka 2008/2009 (10,619 wakiwa wanawake) hadi wanafunzi 51,840 kwa mwaka 2012/2013. Ongezeko hili limechangiwa na uamuzi
wetu wa kutoa mikopo na ufadhili kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi ambapo fani
za Sayansi ya Tiba, Uhandisi, Sayansi za Asili (natural sciences) na Kilimo
zimepewa kipaumbele. Pia limewezekana kwa kufanya uamuzi wa kupanua udahili
katika vyuo vyetu vikiwemo Chuo Kikuu kipya cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Madaktari
Muhimbili. Halikadhalika tumekifanya Chuo
cha Ufundi Dar es Salaam na Chuo cha Ufundi cha Mbeya kuwa vyuo vikuu yaani Dar
es Salaam Institute of Technology na Mbeya University for Science and
Technology. Tukafanya pia uamuzi wa kuanza kujenga Kampasi mpya ya Kufundishia
ya Chuo Kikuu cha Muhimbili pale Mloganzila ambapo kitakapomalizika kitadahili
wanafunzi wa udaktari 12,000 kwa
mwaka. Wakati tunapanua elimu ya sayansi katika ngazi ya vyuo vikuu, tumefanya
hivyo pia katika ngazi ya mafundi mchundo (technicians) kwa kupanua elimu ya
vyeti na stashahada katika elimu ya ufundi. Tumeongeza ujenzi wa Vyuo vya
Ufundi (VETA) kutoka 21 mwaka 2005
hadi 28 hivi sasa. Kutokana na upanuzi
huu udahili wa wanafunzi katika vyuo hivi umeongezeka kutoka wanafunzi 13,650 mwaka 2005 hadi kufikia 49,329 hivi sasa. Aidha, katika kipindi hiki pia tunasomesha ndani
na nje ya nchi zaidi ya wanafunzi 100 masomo ya gesi asilia na mafuta kwa ajili
ya kujenga uwezo wetu wa ndani wa kusimamia sekta ya gesi na mafuta.
Uandaaji
wa Wanasayansi Katika Ngazi ya Awali
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Ndugu Wahitimu;
Tatizo tulilolibaini
katika uendelezaji wa sayansi nchini ni msingi dhaifu tuliokuwa nao wa
kuwaandaa wanasayansi katika ngazi za awali za elimu yetu. Tukajiuliza kwa nini
wanafunzi wetu wanayakimbia masomo ya sayansi na hisabati na ufaulu wamasomo
haya unashuka? Tukabaini matatizo matatu: Kwanza, upungufu wa waalimu wenye
sifa za kumudu kufundisha masomo ya sayansi; pili, uhaba wa vitabu vya masomo
ya sayansi katika shule zetu za sekondari, na tatu ukosefu wa maabara. Tathmini
ilionyesha tulikuwa na upungufu wa waalimu ya sayansi 23,500 mwaka 2013 wakati uwezo wa vyuo vyetu ni kuzalisha waalimu 2,500 tu kwa mwaka. Tumechukua hatua za kuongeza kasi ya
upatikanaji wa walimu wa sayansi kwa ajili ya shule zetu. Hatua mojawapo ambayo tumechukua ni kuongeza
nafasi 5,000 za wanafunzi wa kusomea
stashahada maalumu ya ualimu wa masomo ya sayansi kwa mwaka 2014/2015 katika
Chuo Kikuu cha Dodoma. Tumefanya uamuzi wa kuwawezesha wanafunzi hao kupata
mikopo ya Serikali.
Kwa upande wa vitabu,
nilielekeza Wizara ya Elimu kuainisha fedha za vitabu katika bajeti yake na
kuhakikisha kwamba fedha hizo zinatumika kwa ajili ya vitabu. Aidha, niliwaomba
marafiki zetu wa Marekani na wakakubali kutuchapishia vitabu milioni 2.1 vya sayansi na hisabati ambavyo
vilikwishasambaza mashuleni katika awamu ya kwanza. Katika awamu ya pili wametuchapishia vitabu milioni 2.5 ambavyo Wizara
imekwishavipokea na nimeagiza visambazwe mara moja mashuleni. Baada ya kugawiwa kwa vitabu hivi tatapunguza
tatizo la vitabu vya sayansi kutoka wastani wa kitabu kimoja kwa wanafunzi wanne
(1:4) mwaka 2009 hadi kufikia kitabu
kimoja kwa wanafunzi wawili (1:2). Lengo letu ni kufikisha wastani wa kitabu
kimoja kwa mwanafunzi mmoja (1:1).
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Kuhusu tatizo la
maabara, mwezi Novemba, 2012 nilifanya uamuzi wa kujenga maabara za masomo ya
kemia, fizikia na baiolojia katika shule zetu za sekondari ili kuwezesha
wanafunzi wetu kusoma kwa vitendo. Huku nako kulikuwa na changamoto kubwa sana.
Wakati tunapanua elimu ya sekondari kupitia Mpango wa Elimu ya Sekondari (MMES)
na hasa ujenzi wa sekondari za Kata tuliongeza idadi ya shule kutoka 828 mwaka 2004 hadi shule 3,551 hivi sasa. Nyongeza hii kubwa
imetokana na mchango wa wananchi. Wamechangishana
chochote walichokuwa nacho na kujitolea nguvu za kujenga madarasa, ofisi za
shule na nyumba za walimu. Bahati mbaya tulipokuwa
tunahimiza ujenzi wa shule za sekondari za kata
tulikazania kujenga madarasa tukasahau ujenzi wa maabara. Tukajikuta
kati ya shule 3,551 za sekondari, ni
shule 88 tu (hizi ni zile shule za
kongwe) ndiyo zilikuwa na vyumba vitatu vya maabara za kemia, baiolojia na
fizikia kila moja. Hivyo tathmini ilionyesha kuwa tunahitaji kujenga maabara
kwenye shule 3,463 yaani vyumba vya
maabara 10,389. Ujenzi uliendelea
lakini haukuwa na kasi ya kuridhisha. Ndipo Novemba, 2012 nikatoa agizo la kila
shule ya sekondari ya kati iwe imejenga maabara za fizikia, kemia na bailojia ifikapo
mwezi Novemba, 2014.
Agizo langu hilo
limewazindua wananchi na viongozi na kuongeza msukumo wa ujenzi wa maabara za
sayansi. Taarifa za awali nilizopata wakati nikisubiri taarifa ya tathmini
kutoka TAMISEMI inaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 7, 2014, vyumba 3,867 vya maabara sawa na asilimia 37.2 vilikuwa vimekamilika,
vyumba 5,891 sawa na asilimia 56.7 vilikuwa katika hatua
mbalimbali za ukamilishaji na vyumba 631
tu sawa na asilimia 6.1 ndiyo
ambavyo ujenzi wake ulikuwa haujaanza. Natoa pongezi za dhati kwa viongozi na
wananchi wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Kwa ajili ya kumaliza palipoishia nawaongezea
miezi sita. Tumechukua
hatua pia kwa upande wa vitabu vya kiada ambako tulikuwa na upungufu
mkubwa kutokana na kutotengwa kwa bajeti za vitabu.
Utafiti
Ndugu Mkuu wa Chuo,
Eneo jingine ambalo
tulilazimika kulipa msukumo maalum ni kwenye utafiti, maana sayansi bila
utafiti haiwi kamilifu. Hapa tulikumbana na changamoto tatu kubwa. Kwanza, upungufu wa watafiti katika
vyuo na vituo vya utafiti; pili,
ukosefu wa fedha za utafiti na uchakavu wa miundombinu ya vituo vya utafiti; na
tatu, kukosekana kwa mfumo na
utaratibu wa kuwatambua na kuwazawadia wagunduzi, na kuzifikisha tafiti kwa
watumiaji ili zitumike kuongeza tija na ufanisi. Nilipotembelea vituo vya
utafiti nchini nikakumbana na tatizo la uhaba wa watafiti linalotokana na
waliopo kustaafu, kutoajiri wapya kwa sababu ya kusitishwa kwa ajira, na
motisha ndogo isiyovutia watafiti vijana.
Kwa kutambua umuhimu
wa watafiti na mahitaji yetu ya watafiti kwa ajili ya kuleta mapinduzi ya
kilimo nchini na sekta
nyingine, nikafanya uamuzi ufuatao: niliagiza waliofikia umri wa kustaafu
wapewe mikataba ya kuendelea na kazi. Nilielekeza kuwa vituo vipatiwe kibali cha
kuajiri watafiti wapya na kuweka lengo la kutenga asilimia moja ya bajeti ya serikali kila mwaka kwa ajili ya shughuli
za utafiti. Kwa upande wa kutambua wagunduzi na watafiti tulianzisha nishani
maalum.
Fedha za utafiti
zimekuwa zinapelekwa kwenye Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kupanga
mipango ya kufadhili tafiti na kugharamia mafunzo ya watafiti. Uko mfumo pale COSTECH wa utotoaji teknolojia
(technological incubators) ambapo vijana wadogo wanafanya maajabu katika eneo
la TEHAMA. Tukaamua pia kulinda haki za wagunduzi kwa kuanzisha sheria namba 7 ya mwaka 1999 kuhusu hati miliki
(patent) za wanasayansi wetu.
Ujenzi
wa Miundombinu ya Sayansi
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Pamoja na jitihada
zetu za kujenga msingi wa sayansi kwa maana ya wanasayansi, tumefanya hivyo pia
kwa miundombinu muhimu kwa maendeleo ya sayansi. Miongoni mwa hayo ni ujenzi wa
mkongo wa taifa wa mawasiliano (fibre optic) utakaofika kwenye Wilaya zote
nchini. Mkongo huu ndiyo uti wa mgongo
wa kubebea maendeleo ya sayansi na teknolojia ambapo TEHAMA ina nafasi maalum. Tumeshakamilisha
kuunganisha mikoa yote ya Tanzania Bara na mkongo wa taifa, kwa sasa ujenzi
unaendelea kuunganisha mikoa ya Zanzibar.
Aidha, tunaendelea na ujenzi wa mkongo wa taifa hadi tuunganishe wilaya
zote nchini.
Mkongo wa taifa wa mawasiliano
umewezesha gharama za simu kushuka kwa asilimia
57 kati ya mwaka 2009 hadi 2013 na gharama za intaneti kupungua kwa asilimia 75 kati ya kipindi hicho pamoja
na kuongeza kasi ya mtandao kuendana na viwango vya kimataifa. Hii imewezesha
urahisi na unafuu katika utoaji wa huduma za kimtandao zikiwemo huduma za
elimu, afya, fedha na mawasiliano hususan simu ambazo gharama zake zimepungua
sana kutokana na matumizi ya mkongo huo.
Hali kadhalika
tumeboresha miundombinu ambayo itasaidia wataalamu wetu kutoa huduma walizokuwa
hawawezi kuzitoa na kwa ubora zaidi. Tumejenga
Kitengo cha Kisasa cha Maradhi ya Moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
ambacho kina uwezo wa kulaza wagonjwa wa moyo 100 na kufanya operesheni za moyo,
tumejenga Kituo cha Utafiti wa Magonjwa (Diagnostic Centre) pale Chuo
Kikuu cha Dodoma ambacho kimemalizika kinasubiri uwekaji wa vifaa hiki
kitajihusisha pia na tiba ya magonjwa ya figo na sasa tunajenga Kituo cha
Kisasa cha Magonjwa ya Mishipa ya fahamu pale Muhimbili kitakachokuwa na uwezo
wa kufanya upasuaji na kutoa tiba ya magonjwa ya mishipa ya fahamu.
Hitimisho
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Tumefanya mengi sana
katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo pamoja na sayansi na teknolojia
nchini. Nyote ni mashahidi wa juhudi zetu hizi. Idadi ya madaktari, wahandisi,
watafiti na wataalamu wa fani nyingine za sayansi imeongezeka sana. Hata hivyo
hatujaridhika bado maana safari yetu ni ndefu. Tukijitazama wenyewe ni kweli
tumepiga hatua, ila tunapojitazama kwa kujilinganisha na wengine bado tuko
nyuma sana. Tunapaswa kukimbia wakati wenzetu wanatembea. Chuo hiki cha Sayansi
na Teknolojia kina nafasi muhimu katika utekelezaji wa dhamira yetu hiyo.
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali itashirikiana nanyi na kila mdau katika
kukuza sayansi na teknolojia nchini. Naamimi kwa dhati kabisa inawezekana, tena
matokeo yanaweza kuonekana katika kipindi cha uhai wetu.
Kwa maneno hayo
mengi, nawashukuruni tena kwa heshima kubwa mliyonipa ya kunitunuku Shahada ya Heshima
ya Uzamivu ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela. Sitawasahau kwa wema huu na imani hii mlioionyesha
kwangu na Serikali ninayoiongoza. Mmetambua juhudi zetu na kutuvika taji. Kwa
kweli mmetutia moyo na kutuongezea ari ya kufanya maradufu ya ilivyo sasa.
Tutafika safari yetu ya mwaka 2025 tena ikiwezekana kabla ya mwaka huo. Nia tunayo, sababu tunayo na uwezo tunao.
Asanteni kwa
kunisikiliza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...