MWANAMUZIKI mkongwe pia Kiongozi wa bendi ya Twanga Pepeta Luizer
Mbutu amesema katika kupamba usiku wa Luizer Mbutu ikiwa ni
maadhimisho ya miaka 16 ndani ya bendi bila kutoka ataimba nyimbo zote
za bendi ambazo alishiriki kwa namna moja ama nyingine.
Akizungumza na Ripota wetu jana Mbutu alizitaja baadhi ya nyimbo
hizo kuwa ni ‘Kisa Cha Mpemba’, ‘Jirani’, ‘Fainali Uzeeni’, ‘Mtu
Pesa’, ‘Safari 2005’, ‘Mwana Dar es Salaam’ , ‘Kuolewa’ pia kutakuwa
na wimbo maalum siku hiyo.
Mbutu aliongeza kwa kusema kuwa amefurahishwa na wasanii wa kike
kujitokeza katika kutoa sapoti siku hiyo ambapo anamtaja mwanamuziki
aliyeongezeka kuwa ni Hafsa Kazinja, ambaye atajumuika na Stara
Thomas ‘Stara T’, Siza Mazongera ‘Mamaa wa Segere’.
Wengine ambao watanogesha onyesho hilo kuwa ni bendi ya Utalii
inayoongozwa na Komandoo Hamza Kalala ‘Mzee wa Mdaongo’, bendi ya
Msondo Ngoma .
Wakati huohuo Mbutu alisema kwamba naye waliokuwa wanenguaji wakali
wa bendi ya hiyo Lilian Tungaraza ‘Lily Internet’ na Aisha Madinda
nao watakuwepo siku hiyo ambapo wataudhihirishia umma kwamba bado wako
gado.
Mbutu alisema kwamba pia mwanamuziki ambaye aliwahi kufanya kazi
katika bendi hiyo Roggert Hegga ‘Caterpiller’ , Bob Gaddy Wai na
Ramadhan Masanja wamethibitisha kuwepo katika maadhimisho hayo
yatakayofanyika Desemba 20 katika ukumbi wa Mango Garden Kindoni
Jijini Dar es Salaam kwa kiingilio cha sh.10,000.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Asha Baraka alisema kuwa wameandaa
onyesho hilo ambalo litakua maalum kwa Kiongozi wa bendi hiyo ambaye
anaetimiza miaka 16 ndani ya bendi bila kuhama tangu ilipoanzishwa
hivyo wanafanya hayo ikiwa ni katika kuenzi mchango wake ndani ya
bendi.
“Uongozi wa ASET umeamua kuandaa usiku maalum wa kumuenzi Luiza
kutokana na kua na msimamamo wa kukaa katika bendi kwa muda wote huo
bila kuhama hilo ni jambo la kujivunia” alisema Mkurugenzi wa bendi
Asha Baraka.
Pia aliongeza kwa kusema kuwa wao kama ASET wanatambua mchango wa
Luiza ndani ya bendi hiyo hivyo kutakuwa na tukio la aina yake ambalo
mashabiki na wadau wa bendi hiyo pamoja na wapenzi wa Luiza wajitokeze
kwa wingi siku hiyo kushuhudia litakalojiri sambamba na kupata
burudani kutoka kwa bendi ya Twanga Pepeta.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...