Baada ya mapumziko ya karibu miezi miwili, vumbi la Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuanza kutimka tena kuanzia jumamosi hii kwa pambano moja litakalochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kwa kuzikutanisha timu za Simba na Kagera Sugar. Simba ambayo imelitumia vyema dirisha dogo la usajili kwa kufanya usajili wa baadhi ya nyota kuimarisha kikosi chao itaivaa Kagera ikitokea Zanzibar ilipokuwa imeweka kambi yao tangu Jumapili iliyopita.

Mabingwa hao wa zamani katika dirisha dogo imewaongeza kikosini, nyota kutoka Uganda, Dan Sserunkuma na mdogo wake, Simon Sserunkuma na beki Juuko Mursheed sambamba na beki wa pembeni kutoka Mtibwa Sugar, Hassan Kessy.

Timu hiyo ambayo katika mechi saba zilizopita iliambulia ushindi mmoja tu dhidi ya Ruvu Shooting ikiwa ni baada ya miezi nane ya kucheza bila kushinda tangu msimu uliopita itakuwa na kazi nguvu mbele ya Kagera ambayo katika dirisha dogo la usajili haikusajili mchezaji yeyote na rekodi yake mbele ya Simba kila wanapokutana jijini Dar es Salaam inawabeba.

Kwa misimu miwili mfululizo timu hiyo imekuwa ikiiwekea nguvu Simba kwenye uwanja wa Taifa, jambo linalotarajiwa kutokea hata katika mchezo huo kutokana na maandalizi iliyofanya timu hiyo chini ya kocha kutoka Uganda Jackson Mayanja.

Katika msimu wa 2012-2013 timu hizo zilitoshana nguvu ya kufungana mabao 2-2 na msimu wa mwaka jana matokeo yaliishia kwa sare ya 1-1 na kuibua vurugu kubwa kutoka kwa mashabiki wa Simba waliokuwa hawajafurahishwa na bao la kusawazisha la wapinzani wao.

Katika mechi hiyo, Simba wanashuka dimbani wakiwa nafasi ya saba katika msimo wa ligi wakiwa na pointi tisa mkononi tofuati na mahasimu wao Yanga ambao wanashika nafasi ya tano.

Mechi nyingine zitakazochezwa siku hiyo ni Mtibwa Sugar na Stand United kuonyeshana kazi katika uwanja wa Manungu, mjini Morogoro, Prisons-Mbeya itaikaribisha Coastal Union mjini Mbeya huku JKT Ruvu na Ruvu zitatoshana nguvu kwenye uwanja wa wa Chamazi huku Jumapili Mbeya City ikiikaribisha Ndanda 'Kucheree' uwanja wa Sokoine-Mbeya, Polisi Moro kuialika Mgambo JKT kwenye uwanja wa Jamhuri-Morogoro na wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa Yanga na Azam zitaonyeshana ubabe kwenye uwanja wa Taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...