Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw.
Jumanne Sagini akiwaeleza waandishi wa Habari kuhusu utaratibu utakaotumika
hapo kesho wakati wa upigaji kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo
vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa mbili asubuhi (2:00) hadi saa kumi
alasiri (10:00) ambapo wananchi wote watakaokuwepo vituoni hadi kufikia muda
huo wataruhusiwa kupiga kura hadi watakapokuwa wamemalizika.Kushoto ni Mratibu
wa uchaguzi huo bw.Denis Bandisa
FRANK MVUNGI-MAELEZO
Serikali imewataka wananchi wote
waliojiandikisha kupiga kura katika
uchaguzi wa Serikali za Mitaa kushiriki
kwa wingi ili waweze kuwachagua viongozi wao katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Ofisi
ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Jumanne
Sagini wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam .
Akifafanua Sagini amesema wapiga kura
wazingatie kuwa kila mpiga kura anatakiwa kupiga kura moja tu na apige kwenye
kitongoji au mtaa anaoishi na si
vinginevyo.
Pia Sagini alitoa wito kwa viongozi wa
vyama vya siasa, Asasi zisizo za Kiserikali kuwahamasisha wapiga kura
kujitokeza kwa wingi hapo kesho kuchagua viongozi wao.
Akiwatahadharisha wananchi kuhusu kupiga
kura Zaidi ya mara moja au kutaka kupiga kura wakati si mkazi wa eneo hilo Sagini alisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale
wote watakaojaribu kukiuka sheria, Kanuni na taratibu za uchaguzi huo.
Katika uchaguzi huo sagini alibainisha
kuwa utaratibu utakaotumika ni kupiga kura,kuhesabu na kutangaza matokeo ambapo
taratibu zote zimefafanuliwa katika Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za
mwaka 2014 na katika mwongozo wa uchaguzi huo.
Wapiga kura wote wametakiwa kufika
katika maeneo ya kupigia kura wakiwa na kitambulisho cha mpiga kura cha
Uchaguzi Mkuu, Kitambulisho cha kazi,Hati ya kusafiria,Kadi ya benki,Kadi ya
Bima ya Afya,Kitambulisho cha shule au chuo,Leseni ya Udereva au Kitambulisho
cha uraia kwa ajili ya kuwatambulisha.
Uchaguzi wa Serikali za mitaa katika
ngazi za vijiji,Mitaa na vitongoji utafanyika siku ya jumapili ya tarehe 14
Desemba,2014 ambapo katika uchaguzi huo watachaguliwa wenyeviti wa vijiji na
wajumbe wa Halmashauri za Vijiji,Wenyeviti wa Mitaa na wajumbe wa Kamati za
mitaa na wajumbe wa kamati za Mitaa na wenyeviti wa vitongoji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...