Umoja wa wamiliki magari ya mizigo TATOA umewapa
pole wamiliki wa magari, madereva na wafanya biashara wanaosafirisha mizigo
kuelekea Kongo DRC kufuatia ajali ya moto iliyotokea takribani wiki mbili
zilizopita katika Yadi ya Whiski iliyoko jirani na mpaka wa Kasumbalesa katika
nchi ya Demokrasia ya watu wa Kongo na kusababisha vifo na uharibifu wa mali.
‘TATOA inatoa pole kwa familia na waathirika wote
wa janga hili la moto kutoka nchi za Tanzania, Zambia, Zimbabwe, Congo na
Afrika Kusini, na pia kipekee TATOA inapenda kutoa shukrani kwa serikali ya
Congo kwa juhudi zao za kuhakikisha hali ya amani boda na kazi kuendelea pamoja
na taratibu mpya za kiusalama walizochukua’ alisema msemaji wa TATOA, Bwana
Elias Lukumay.
Akielezea chanzo cha moto huo, bwana Lukumay alisema
taarifa za awali zinaonyesha mlipuko huo ulitokea baada ya gari la mafuta
kukwaruza gari jingine hivyo kupata nyufa katika Tanki lake la mafuta
hali iliyosabababisha mafuta kuvuja na kutapakaa katika eneo la Yadi na
baadaye kushika moto.
‘Tatizo la msingi ni kuwa yadi ya
Whiski haikuwa na vifaa vya kupambana na moto, na hivyo tunaziomba serikali
zetu zinazosimamia vituo vya mipakani kujifunza kutokea kwenye tatizo hili na
hivyo kuchukua hatua stahiki kuboresha huduma kwenye yadi hizo’ alisisitiza
Lukumay.
Bwana Lukumay pia alisema TATOA imetuma timu ya
wataalam kwenda Lubumbashi kuangalia upana wa maafa, huku pia IKITOA wito kwa
makampuni mwanachama wa TATOA kutoa taarifa kuhusiana na maafa waliyoyapata.
‘TATOA, ingependa kuona inapata ushirikiano wa karibu kutoka upande wa
serikali, ili kwa pamoja tujipange na tuweze kufanya maandalizi ili janga kama
hili lisije tokea kwenye boda zetu zote siku zijazo’ alisema Lukumay.
TATOA pia imeiomba mamlaka ya barabara Tanzania
(TANROADS) kupunguza usumbufu usio wa lazima kwa malori katika maeneo ya mizani
hasa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ambapo bandari yetu imejaa mizigo
mingi ya nchi jirani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...