Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imemteua Dk Kassim Hussein kuwa mwenyekiti wa muda wa bodi ya wakurugenzi.

Hatua hiyo imetokana na kuteuliwa kwa aliyekuwa mwenyekiti wa bodi ya benki hiyo, Profesa Mussa Assad, kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . 

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Muda wa NBC, Bwana Pius Tibazarwa alisema Dk Hussein atashika wadhifa wa uenyekiti wa bodi ya benki hiyo mpaka pale atakapoteuliwa mwenyekiti wa kudumu wa bodi hiyo.

Dk Hussein ni mhadhiri mwandamizi katika masomo ya kibenki na ya fedha katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (Institute of Finance Management – IFM) cha Dar es Salaam. Dk Hussein ni msomi mwenye Digrii ya Uzamivu katika masomo ya kibenki na Digrii ya Uzamili katika masomo ya fedha. Aliteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya Wakaurugenzi wa NBC tangu mwaka 2010.

“Kwa mara nyingine tena, tunampongeza Profesa Assad kwa kuteuliwa kwake na kumtakia kila la kheri katika kazi hiyo. Tunamshukuru pia kwa utumishi wake uliotukuka katika kipindi chake kama mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya NBC. 

NBC itaendelea kushirikiana nae kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika sekta ya fedha hapa nchini. Wakati huo huo, tunamtakia kila la kheri Dk Hussein katika nafasi yake mpya ya uenyekiti wa bodi ya NBC,” alisema Tibazarwa.

Profesa Assad aliteuliwa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania mnamo mwezi Novemba 2014 baada ya kuitumikia NBC kama mwenyekiti wa bodi tangu mwaka 2006.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...