Na Bashir Yakub
Katika shughuli zetu za kuuza na kununua ambazo tunazifanya kila siku mikataba ya maandishi ni jambo ambalo wengi tunakutana nalo. Mikataba hii iwe rasmi au isiwe rasmi suala la msingi ni kuwa huwa tunaifanya. Aidha wakati mwingine si wote wenye kuhusisha suala la mikataba ya maandishi katika makubaliano yao mbalimbali na hii hutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kuaminiana.
Kuhusu kuaminiana niseme jambo moja tu kuwa suala la mikataba ni muhimusana hata kana mwenzako unamuamini kwa kiwango cha juu kabisa( highest degree of trust). Nathubutu kusema kuwa hata awe mzazi wako kama kuna jambo la msingi mmelifanya ni vema kukawapo mkataba wa maandishi.
Nasema hivi kwakuwa kwa uzoefu wangu wa mambo haya mara nyingi mgogoro hautokani na waliouziana au kukubaliana isipokuwa mgogoro unakuja kuanzishwa na walio nyuma ya hao. Kwa mfano baba anaweza kumpa mwanae kiwanja na wasifanye mkataba wowote wa maandishi kwa kuwa wanaaminiana.
Hiyo ikaenda kwa miaka kadhaa ambapo baba akawa amefariki. Baaada ya hapo anaibuka mtu anasema mimi ni mtoto wa marehemu kwa hiyo nahitaji kiasi kadhaa kutokamali hii. Hapa mgogoro si kati ya baba na mwana tena isipokuwa ni kati ya mwana na mtu mwingine. Kama huna mkataba wowote wa maandishi mpaka kesi hii kuisha waweza kuwa umepoteza kila kitu.
Huu ni mfano tu katika kusisitiza kuwa mtu asiseme mi na fulani tunaaminiana. Mgogoro sio lazima utokane na nyie wawili isipokuwa walio nyuma yenu waweza kuanzisha mgogoro.
MADHARA YA KUTOFANYA MKATABA WA KISHERIA .
Ni vema sana kujihadhari kwakuwa ukisikia neno mgogoro ujue kuna mambo makubwa mawili.
Kwanza gharama kubwa ni uwezekano wa kupoteza kabisa ilemali na haijalishi iwe uliinunua au ulipewa isipokuwa tu ukishakuwa na mgogoro upo katika hatari hiyo. Pia gharama ya pesa kama kuwalipa wanasheria, gharama za uendeshaji kesi, nauli na matumizi mengineyo ambayo hujitokeza bila hata kutarajia.
Pili kuna gharama ya muda . Hii huhusisha kushinda mahakamani kila siku na wote mwajua mahakama zetu zilivyo, kushinda vituo vya polisi huku shughuli zako za msingi za kila siku zikisimama. Pia hapa kuna muda wa kusubiri hukumu ambapo kesi yaweza kukaa mahakamani hata miaka sita . Hakika unakuwa umesurubika(suffer) na umepoteza mambo mengi katika kushughulikia jambo hili.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...