![]() |
Katibu Mkuu wa CCM Ndugu
Abdulrahman Kinana pamoja na viongozi wengine wa CCM na wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar wakiwa nyumbani alipozaliwa marehemu Issa Ahmed Othman
Mshauri wa Rais Zanzibar katika masuala ya Utalii,aliyefariki nchini India alipoenda
kwa matibabu.
Katibu Mkuu alitoa salaam za pole kwa familia ya marehemu na ndugu
zake kupokelewa na kaka wa marehemu Othman Ahmed Othman nyumbani kwao Shenge
Juu, Pemba.
|
Na
Abdulla Ali - Maelezo, Zanzibar
Aliyekuwa
Mshauri wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika mambo ya Utalii Mhe.
Issa Ahmed Othman amefariki dunia baaada ya kuugua kwa muda mrefu.
Marehemu
Issa Ahmed alifariki siku ya tarehe 25/01/2015 akiwa katika matibabu nchini India
na amezikwa jana katika kijiji cha Kianga nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ambapo
kifo chake kimeleta mshtuko, huzuni na masikitiko makubwa kwa Chama Cha
Mapinduzi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Marehemu
alizaliwa mnamo tarehe 24 Julai, 1951 katika kijiji cha Pandani Wilaya ya Wete,
Mkoa wa Kaskazini Pemba na kupata elimu yake ya msingi katika Skuli ya Pandani
Pemba na baadae kupata elimu ya sekondari Uweleni Pemba na kufaulu kidato cha
nne pamoja na masomo ya Qur-aan aliyoyapata hapohapo kijijini kwao.
Katika
jitihada za kupanua elimu yake Marehemu alijiunga na Chuo cha Uhasibu na
kufaulu kuwa mhitimu wa Taaluma ya Uhasibu katika ngazi ya Stashahada.
Kwa
upande wa utumishi Marehemu alishika nyazifa mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar zikiwemo; Mkaguzi wa Ndani (1969-1974), Mhasibu Wizara ya Biashara
Pemba (1975-1984), Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi (1985-1995), Naibu Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Maliasili Zanzibar (1988-1995), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
ya Shirika la Bima Zanzibar (1987-2000), Makamo Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi
Shirika la Bandari (1988-1999), Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar
(2000-2010), Mshauri wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika mambo ya Utalii
2010 hadi mauti yalipomfika.
Kwa
upande wa chama, Marehemu alikuwa ni Mwanachama wa Afro Shirazi Party (ASP) na
baada ya kuungana kwa vyama vya TANU na ASP mwaka 1977 akawa Mwanachama mwanzilishi
wa Chama Cha Mapinduzi.
Katika
kuendeleza jitihada zake za kisiasa na kupata ushirikiano mzuri na wanachama
wenzake Marehemu alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama
Cha Mapinduzi nafasi ambayo ilimjengea umaarufu na kumuwezesha kushika nafasi
za juu za Uongozi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Chama
Cha Mapinduzi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua mchango mkubwa wa Marehemu
Issa Ahmed katika Utumishi na Uongozi wa Chama hicho katika maisha yake kwa
kuwa alikuwa ni Kiongozi mwenye Kuheshimu watu, Mchapakazi mahiri, Mweledi na
aliyekuwa akitegemewa na wengi nchini Zanzibar na bila ya shaka kifo cha Marehemu
kimeacha pengo kubwa katika Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa ujumla.
Aidha
Chama na Serikali vimewataka Viongozi, Ndugu, Jamaa na Marafiki wa Marehemu kuwa
na moyo wa subira katika wakati huu mgumu wa maombolezo ya mpendwa wao huyo.
Hadi
kufariki kwake, Marehemu Issa Ahmed Othman alikuwa ni mshauri wa Rais katika
mambo ya Utalii Zanzibar, na ameacha Kizuka 1, Watoto 7, na Wajukuu 25.
Mwenyezi
Mungu aiweke roho ya
Marehemu mahala pema Peponi.
Amin
IMETOLEWA
NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...