Leo wananchi wa Zambia wanafanya Uchaguzi mdogo kumchagua Rais wa sita tangu wa nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1964. Uchaguzi huu unafanyika kufuatia kifo cha Rais Michael Chilufya Sata, kilichotokea tarehe 28 Oktoba 2014, mjini London Uingereza alikokwenda kwenye matibabu. Rais Sata aliingia madarakani Septemba 2011.

Mshindi katika uchaguzi huu atatawala hadi 2016 ambapo utafanyika Uchaguzi Mkuu.

Katika uchaguzi huu wagombea kutoka vyama vya siasa vipatavyo kumi na moja (11) wamejitokeza kushiriki kama ifuatavyo:

Mhe. Edgar C. Lungu – Chama cha Patriotic Front (PF) –mpaka anapoingia kwenye kinyangányiro hiki ni Waziri wa Sheria na Waziri wa Ulinzi. Yeye anajaribu kutetea chama hiki tawala ili kimalizie kipindi kilichobaki.

Bw. Hakainde Hichilema - Chama cha United Party for National Development (UPND) - ambaye anajaribu tena kwa mara ya nne, anachuana vikali na mgombea wa chama cha PF. 

Dkt. Nevers S. Mumba - Chama cha Movement for Multi Party Democracy (MMD)- mgombea wa  chama hiki ana changamoto kubwa hasa baada ya wengi wa Wabunge wa chama chake kuamua kumuunga mkono mgombea wa chama cha UPND.

Bw. Elias Chipimo (jnr) - National Restoration Party (NAREP) - ambaye anashiriki kwenye uchaguzi kwa mara ya pili sasa. 

Dkt. Ludwig S. Sondashi - Forum for Democratic Alternatives (FDA) - anashiriki kwa mara ya kwanza. Mgombea ni Daktari ambae anasema anatengeneza dawa za ukimwi na ameahidi wapiga kura kutoa dawa yake hiyo bure endapo atachaguliwa.                         

Bibi  Edith Z. Nawakwi - Forum For Democracy and Development (FDD) -  ni mgombea pekee mwanamke na mara yake ya tatu kuingia kwenye kinyang’anyiro cha Urais.

Bw. Tilyenji Kaunda - United National Independence Party (UNIP)- ni mtoto wa muasisi wa Chama hiki kilichoipatia Jamhuri ya Zambia uhuru wake kutoka kwa mkoloni, Mhe. Dkt Keneth David Kaunda. Tangu kiondolewe madarakani 1991, kimeendelea kushiriki kwenye chaguzi hizi bila ya mafanikio ya kurudi tena madarakani.

Brig. Jen. (Rtd) Godfrey Miyanda - Heritage Party (HP) - anaingia kwenye kinyang’anyiro kwa mara ya  tatu.

Bw. Daniel M. Pule - Christian Democratic Party (CDP)--- anagombea kwa mara ya kwanza. 

Bw. Peter C. Sinkamba - Green Party- ni mgombea machachari  ambaye anasema akipewa madaraka haya ya juu atafanya bangi kuwa zao halali la biashara. Ana uhakika kuwa serikali itapata mapato makubwa kutoka kwenye bangi hivyo kuondoa tegemezi kwenye zao moja tu la shaba.

Bw. Eric M. Chanda – Chama cha 4th Revolution - Chama hiki kinaingia kwenye uchaguzi wa Rais kwa mara ya kwanza.

Ujumbe wa Waangalizi kutoka nchi wanachama wa SADC uliopo Lusaka, Zambia akiwemo Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Grace J. Mujuma umetembelea vituo vya uchaguzi asubuhi hii na kukuta watu wamejipanga kwenye vituo hivyo tangu majira ya saa kumi na moja asubuhi. 

Kituo cha kwanza ambacho kilitembelewa na ujumbe huu kilifunguliwa rasmi saa 12 asubuhi kukiwa na wahusika wote na kulingana na taratibu zilivyopangwa na Tume ya Uchaguzi wa Zambia na uchaguzi kuendelea kwa hali ya shwari.

 UBALOZI WA TANZANIA
LUSAKA, ZAMBIA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...