Na Mwandishi Wetu

Wasanii nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kutoa elimu ya uraia kwa wananchi ili watambue umuhimu wa kupiga kura na kuwaweka madarakani viongozi wanaowataka.

Wito huo umetolewa mapema wiki hii na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa  (BASATA) Godfrey Mngereza wakati akichangia mada kuhusu Umuhimu wa Jamii kupiga kura kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika makao makuu ya BASATA Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.

“Kama taifa tunazungukwa na matukio mengi yanayohitaji wananchi kupiga kura katika kuamua. Tuna tukio la kupiga kura ya maoni juu ya katiba inayopendekezwa lakini pia uchaguzi mkuu. Wasanii tuna wajibu wa kuwajengea hamasa wananchi kushiriki matukio haya muhimu” alisisitiza.

 Aliongeza kwamba wasanii hawana budi kutambua kwamba wana nafasi kubwa kuhakikisha wanawaelimisha wananchi kuhusu nafasi waliyonayo katika kuamua hatma yao lakini pia kuwa katikati katika kuibua masuala mbalimbali yaliyoko katika jamii ili kuwapa wananchi uchaguzi sahihi linapokuja suala la kupiga kura.

“Wasanii hampaswi kuwa na upande mnapotoa elimu bali wajibu wenu ni kuibua na kuielimisha jamii kuhusu upigaji kura. Suala la nani apigiwe kura na wananchi linabaki kuwa mikononi mwa mwananchi mwenyewe ambaye ndiye mpiga kura” aliongeza.

Awali, wakitoa burudani kwenye Jukwaa hilo la Sanaa, wasanii kutoka kundi la Bongo Artists Foundation linaloongozwa na msanii wa maigizo Christian Kauzeni walitoa elimu mbalimbali kuhusu umuhimu wa wananchi kupiga kura huku wasanii hao wakionesha kwa hisia kali madhara yatokanayo na wananchi kutokupiga kura.

Kundi hilo lililovuta hisia za wadau takribani themanini waliohudhuria kwenye Jukwaa la Sanaa lilionesha madhara ya kutokupiga kura kuwa ni pamoja kupatikana kwa viongozi wabovu wasiyowajibika,kukosekana kwa huduma muhimu za jamii na changamoto nyingine nyingi ambazo zinakwamisha jitihada za wananchi kujikwamua kutoka kwenye ufukara.
Kiongozi wa Kundi la Bongo Artists Christian Kauzeni (Katikati) akizungumza na wadau wa Jukwaa la Sanaa (hawako pichani) wakati Kundi lake lilipotoa elimu kupitia Sanaa za Majukwaani kuhusu umuhimu wa wananchi kupiga kura mapema wiki hii. Kulia ni Afisa Habari wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Aristide Kwizela na Afisa Sanaa wa baraza hilo Ernest Biseko.
Moja ya wasanii wa Bongo Artists akiwauliza swali la Je kutokupiga kura ni uhayawani? Wadau wa Jukwaa la Sanaa wanaomtazama. Msanii huyu alikuwa kivutio kikubwa hasa kwa kuuliza swali hilo la Je Huu ni Uhayawani? Ambalo lilienda sambamba na maudhui ya igizo la kundi hilo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Wasanii Tanzania hasa wa filamu na muziki lazima tukubali kuwa mambo yote tunayojaribu kuyajadili mfano; elimu ya upigaji kura tunadanganyana tu. Tunaiga maudhui ya nchi za magharibi kisanaa alafu tunatenda ya nchi maskini. Hapo jamaa ameongelea wasanii wasiegemee upande mmoja...mbona tayari makundi ya wasanii wa bongo hiphop na bongo flavor wameshatamka kuwania ubunge ktk vyama mbalimbali hapo hapo tanzania.sasa rafiki za ambao ni wasanii si wataegemea vyama vya marafiki zao wakati wa uhamasishaji wa elimu ya kupiga kura. Tuende na wakati. Nchi za magharibi hamna hili la wasanii kutoa elimu ya upigaji kura. Mambo ya zamani sana hayo ndugu mngereza. Kwanza tatueni haki miliki za wasanii, tatueni jinsi ya wao kupata malipo yao halali ya kazi zao. 'Msihimize kulima kwa matrekta ili hali hata jembe la mkono kulishika hamjui' tanzania na mambo yake kisiasa tunayafahamu, kesho CCM wanawalipa wasanii hao hao kupamba kampeni zao, leo mnawaambia watoe elimu ya upigaji kura. Wapi na wapi? Mdau USA

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...