Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu (aliyenyoosha mkono),
akimwonyesha Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene,
jinsi maji ya bahari yalivyoathiri eneola MnaziBay, karibu na kampuni ya
kuzalisha umeme ya Maurel & Prom.
.jpg)
Athari ya mmomonyoko wa ardhi katika eneo la MnaziBay inavyoonekana
pichani. Mmomonyoko huo umetishia usalama wa Kiwanda cha kufua
umeme unaotumiwa na wakazi wa Lindi na Mtwara cha Maurel & Prom.
Na Veronica Simba aliyekuwa Mtwara
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu ameushukuru uongozi wa
Wizara ya Nishati na Madini kwa ushirikiano ilioonyesha katika zoezi
linaloendelea kudhibiti kasi ya maji Pwani ya Mnazi Bay, yaliyosababisha
mazingira ya hatari kwa bomba la gesi na kiwanda cha kuchakata gesi
asilia cha Maurel & Prom.
Alitoa shukrani hizo hivi karibuni wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati na
Madini, George Simbachawene mkoani humo kukagua miradi mbalimbali
inayosimamiwa na Wizara yake hususan Mradi wa bomba la gesi asilia
kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
“Kazi iliyofanyika imewezesha kudhibiti kasi ya maji kuendelea kumega
sehemu ya ardhi iliyobaki. Kazi ya kudhibiti kingo za bahari inaendelea
vizuri na tunashukuru uwezeshaji wa haraka uliofanywa na Wizara na
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),” alisema Dendegu.
Akielezea hali halisi iliyopo sasa baada ya jitihada zilizofanywa kukabiliana
na janga hilo, Dendegu alisema kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha
Mnazi Bay kinachoendeshwa na kampuni ya Maurel & Prom, kinaendelea
kuzalisha gesi na Mikoa ya Lindi na Mtwara inaendelea kupata umeme.
Kwa upande wake, Waziri Simbachawene alipongeza jitihada zilizofanywa
na uongozi wa Mkoa wa Mtwara kusimamia zoezi zima la kuzuia
mmonyoko wa ardhi katika kingo za bahari, Pwani ya Mnazi Bay.
“Nawapongeza wenzetu, mmejitahidi. Mmefanya kazi kubwa kuokoa mali
ya taifa,” alisema.
Janga hilo la mmomonyoko wa ardhi, Pwani ya Mnazi Bay lilitokana na
mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na kusababisha kujaa kwa maji
katika Pwani hiyo tofauti na hali ilivyo siku zote.
Kujaa huko kwa maji kulisababisha mazingira ya hatari kwa bomba la gesi
la inchi 16 ambapo ilibakia mita nne tu maji hayo kulifikia bomba hilo.
Aidha, hali hiyo ya kujaa maji pia ilisababisha mazingira ya hatari kwa
kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Mnazi Bay kinachoendeshwa na
kampuni ya Maurel & Prom Tanzania (M&P) ambapo zilibaki mita 29 tu
maji kufikia kiwanda hicho.
Kiwanda hicho ndicho kinachochakata gesi inayoendesha mitambo ya
Tanesco iliyopo Mtwara Mjini na umeme wake kutumiwa na wananchi wa
mikoa ya Lindi na Mtwara.
Makundi ambayo yamekuwa mstari wa mbele kushirikiana kukabiliana na
janga hilo ni pamoja na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la
Polisi, na Jeshi la Magereza.
Mengine ni Kampuni ya Dangote, Kampuni ya Maurel & Prom Tanzania,
Shirika la Petroli Tanzania (TPDC), Wizara ya Nishati na Madini na
Wataalam kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...