Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe
26/01/2015 Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilisaini mkataba maalum
na timu ya Real Madrid ya Nchini Hispania
ya kuanzisha na kuendesha kituo cha michezo (NSSF- REAL MADRID Sports Academy) kwa lengo la kuibua, kuendeleza
na kukuza vipaji kwa mpira wa miguu.
Shirika la NSSF litajenga kituo hicho
katika eneo la Mwasonga Kigamboni nje kidogo ya mji wa Dar es Salaam na
wataalamu kutoka timu ya Real Madrid watatoa mafunzo kwa vijana wa umri wa
miaka13 hadi 19 kwa madhumuni ya kukuza mpira wa miguu nchini, kupata wachezaji
bora wanaouzika nje na ndani ya nchi pamoja na kulipatia mapato shirika na nchi
kwa ujumla .
Akizungumza na Waandishi
kutoka vyombo mbalimbali vya Habari Nchini, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Dr.
Ramadhani K. Dau alisema mradi huo ukiwa kama sehemu ya uwekezaji wa NSSF
ulianza maramoja baada ya kusaini mkataba.
NSSF imeanza utaratibu wa kuwabaini vijana
walengwa ambapo kwa kuanzia utafutaji wa vipaji vya mpira wa miguu utaanzia
mkoa wa Dar es Salaam kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 14. Utafutaji wa vipaji
utafanyika kiwilaya kwa Wilaya za mkoa wa dar es salaam na utakuwa
unafanyika katika viwanja vya Karume. Zoezi
hilo litakuwa linafanyika kati ya saa 1 asubuhi hadi saa 9 alasiri kwa tarehe zilizoainishwa.
Uandikishaji wa washiriki utakuwa unafanyika siku za
mwisho wa wiki ili kutoathiri wanafunzi watakaopenda kushiriki na utaanza rasmi
tarehe 14 na 15,na tarehe 22 na 23 Februari
2015, na kufuatiwa na michezo ya majaribio tarehe 28 Februari,na Tarehe 1 Machi
2015 kwa wilaya zote za mkoa wa Dar es
salaam ambapo kituo kitakuwa viwanja vya Karume kuanzia saa moja asubuhi hadi
saa 9 alasiri.
Zoezi la Uandikishaji halitahusisha gharama
zozote kwa washiriki, na uandikishaji wa washiriki utafanyika kwa kujaza fomu
maalum na kupewa namba ya ushiriki na kila mshiriki atapata fursa ya kucheza katika
awamu mbili za dakika 30. Kwa kuanzia washiriki watatakiwa kuja na vifaa vyao
vya michezo.
Zoezi la awali litafanywa
na wataalam wa ndani ya nchi ambapo Vijana 500 kati ya wote watakaofanyiwa
majaribio wataingia katika awamu ya pili
ya majaribio na watadahiliwa na wataalamu
kutoka Klabu ya Real Madrid na hatimaye kupatikana vijana 30 amabo ndio
wataingia katika shule maalum ya mafunzo
kwa awamu ya kwanza.
Wakati wa uandikishwaji washiriki watatakiwa kuja na
wazazi/walezi wao wakiwa na vitambulisho vyao,na kijana husika awe na Cheti halisi cha kuzaliwa na kopi yake pamoja na picha mbili za pasport rangi ya blue.Muda wa uandikishaji na
majaribio unaweza kuongezwa kulinagana na mahitaji.
Shirika la NSSF linatoa
wito kwa vijana kujitokeza kwani ni fursa kwao ya kuweza kujiendeleza kimichezo
na kujiajiri katika tasnia hiyo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...