Kampuni ya simu Tanzania (TTCL) imezindua mnara wa mawasiliano katika kata ya Kiegei, wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi hivi karibuni.

Akiongea na wananchi Kiegei, Mkuu wa Biashara  (TTCL) kanda ya Zanzibar Bw. Hussein Nguvu amesema; kwa kutambua umuhimu wa mawasiliano, TTCL pekee ndiyo ipo katika kijiji cha KIEGEI na ipo mstari wa mbele katika kuchangia kufanikisha malengo ya Serikali katika Sekta hii mtambuka kwa maendeleo ya haraka kwa Taifa letu.

Amesema Serikali ina imani kubwa na imeridhishwa na utendaji na ufanisi wa TTCL katika kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi hapa nchini na nje ya mipaka kwenda nchi jirani ndio maana imepewa dhamana ya kuendesha na kusimamia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuinua uchumi wa nchi kupita Sekta hii muhimu ya TEHAMA chini ya usimamizi wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

Ameongeza kwa kumshukuru Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) Bw. Peter Ulanga kwa  juhudi zake katika kusimamia mfuko huu ambo umekuwa ni msaada mkubwa katika kuleta maendeleo kupitia Sekta ya Mawasiliano hasa katika maeneo ya vijijini ambayo bado yapo chini Kiuchumi, Kimaendeleo na Kibiashara.

Naye mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa mnara huo ambaye ni Mbunge wa Nachingwea na waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mhe. Mathias amesema kupatikana kwa mawasiliano hayo ya simu katika kata ya  Kiegei, Wananchi wa eneo hilo wataweza kuwasiliana na pande zote za dunia, fursa ambayo wamekuwa wakiikosa kwa muda mrefu.

Pamoja na hilo vile vile kwa kutumia mawasiliano wataweza  kupata na kutumia taarifa za kibiashara na kiuchumi - katika  masoko  mbalimbali  nchini na duniani, hususani bei za mazao yao na kupata habari za masoko mapya. Hii itawawezesha kupata fursa sawa na watu wa maeneo ya mijini na nchi zingine zinazoendelea ili kuendelea kujenga uwiano sawa wa kupata na kutoa taarifa kwa maendeleo ya nchi na watanzania kwa ujumla.

Katika hafla hiyo mkuu wa wilaya ya Nachingwea Bi. Regina Chonjo aliwasisitiza wananchi wa Kiegei kulinga miundombinu ya mawasiliano ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwa manufaa ya sasa na yajayo.

Kupitia mfuko wa kusimamia utoaji wa huduma ya Mawasiliano kwa wote nchini (UCSAF), TTCL ilipewa jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 20 kwa thamani ya  Tshs 3.4 bilioni.  Lengo likiwa ni kupeleka huduma za mawasiliano  katika maeneo ambayo hayana mawasiliano, ni pamoja na kuhakikisha  wananchi waliopo vijijini wanapata fursa ya kuwasialiana na ndugu, kukuza biashara zao na kujenga uwiano sawa kwa wananchi wote nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mh. Mathias Chikawe (mwenye miwani) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mnara wa mawasiliano wa Kampuni ya Simu ya TTCL katika Kata ya Kiegei, Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Regina Chonjo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe akipiga simu ya Kampuni ya TTCL baada ya kuzindua rasmi mnara mkubwa wa mawasiliano wa Kampuni hiyo katika Kata ya Kiegei, Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.Aliyevaa kofia (kulia) ni Mkuu wa Biashara wa Kampuni ya TTCL, Kanda ya Zanzibar, Hussein Nguvu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...