KAMPUNI YA STAMIGOLD
MGODI WA BIHARAMULO

TAARIFA KWA UMMA
17 Februari, 2015.

Kampuni ya STAMIGOLD Biharamulo ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) inakanusha vikali taarifa zilizotolewa na mtandao wa kijamii unaojulikana kama Jamii Forums mnamo tarehe 15 Februari, 2015 kuwa kuna unyama wa kutisha uliofanyika Mgodi wa Dhahabu Biharamulo tarehe 26 Octoba, 2014.

Mgodi wa Stamigold Biharamulo unakanusha tuhuma zote za mauaji zilizotolewa na Jamii Forums kwani taarifa hizi ni za kutunga na zinalenga kupotosha umma kwa kuuchafua mgodi huu pekee wa Serikali unaoendeshwa na wazawa pamoja na kumchafua mtu mmoja ambaye ni Meneja Mkuu wa Mgodi Mhandisi Dennis Sebugwao.

Maisha ya Binadamu ni kitu chenye thamani kubwa kiasi ambacho kifo cha mtu mmoja ni masikitiko kwa kila mtu. Hakuna mtu yeyote aliyewahi kuuwawa ndani ya Mgodi na Kuzikwa Kinyemela na baadae kufukuliwa na kuzikwa sehemu tofauti kama mtandao wa Jamii Forums ulivyopotosha. Wafanyakazi na Wananchi wanaoishi karibu na Mgodi hawajawahi kuona mwili wa marehemu yeyote aliyeuawa au kukutwa amekufa ndani ya eneo la mgodi.

Vilevile, si kweli kuwa Polisi waliokuwa wanasaidia kulinda eneo la mgodi waliondolewa ili kuficha tuhuma za mauaji zilizotolewa bali, waliondolewa kwa lengo la kupunguza matumizi kutokana na ufinyu wa mtaji uliopo kuendesha mgodi kwani kampuni ilikuwa ikiilipa polisi takribani shilingi milioni kumi na sita (16M TSH) kila mwezi kwa ajili ya kusaidia ulinzi eneo la mgodi.

Baada ya kusitisha mkataba na Polisi mwezi Disemba, 2014; (uzushi huu umetungwa kuwa tukio lilifanyika tarehe 26 Oktoba, 2014 wakati huo huo Polisi wasiopungua 17 walikuwa wakifanya doria kwenye eneo la mgodi); mgodi uliendelea kutumia askari wa SUMA JKT ambao tayari walikuwa na mkataba na mgodi wa kufanya shughuli za ulinzi katika eneo la mgodi kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Kitengo cha Ulinzi hapa mgodini. 

Shughuli zote za ulinzi zimekuwa zikifanywa kwa kuzingatia sheria za nchi na zile za kimataifa hasa za haki za binadamu na Meneja Mkuu wa mgodi hakuwahi kutoa amri ya kuruhusu au kuagiza mtu yeyote kupigwa kama taarifa hiyo ilivyopotosha umma.

Tunaomba umma utambue kuwa mgodi wa Stamigold Biharamulo unaendeshwa na kufanya shughuli zake kwa kuzingatia Sheria zote za nchi, Kanuni na Matakwa mengine yanayowezesha utendaji uliotukuka kwa shughuli kama za uchimbaji wa Madini ya Dhahabu. 

Tangu kuanza kwa mgodi kumekuwepo mahusiano mazuri na Jamii inayotuzunguka. Tunashirikiana na kushirikishana mambo mengi ikiwa ni pamoja na kusaidiana wakati kuna majanga au dharura.ya aina yo yote kijijini au katika maeneo ya mgodi.

Meneja Mkuu wa Mgodi Mhandisi Sebugwao anayetuhumiwa na mtungaji wa taarifa hiyo tayari amekwisha toa taarifa kwenye vyombo vya dola ili sheria iweze kuchukua mkondo wake hivyo ni vizuri Polisi wakapewa nafasi ya kufanya upelelezi wao. 

Kupitia taarifa hii Kampuni ya Stamigold Biharamulo inamtaka Mhariri wa Jamii Forums kuomba radhi kwa wasomaji wa mtandao huo pamoja na kuondoa taarifa hiyo potofu kwenye mzunguko wa mtandao wake. Kampuni ya STAMIGOLD Biharamulo inasisitiza vyombo vya habari kuzingatia weledi wa taaluma ya habari na kuandika habari zenye ukweli bila kupotosha umma, ili kwa kufanya hivyo vyombo hivyo visaidie uwepo wa utengemano na uadilifu .

Imetolewa na:
Idara ya Mawasiliano.
STAMIGOLD Biharamulo
S.L.P 78508 Dar es Salaam. 
Barua pepe: info@stamigold.co.tz 
Tovuti: www.stamigold.co.tz

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...