WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amezindua zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa Biometric Voter Registration (BVR) na kuwataka viongozi wa siasa wawahimize wanachama wao wajitokeze kwa wingi bila kujali tofauti za kiitikadi. 
 Ametoa wito huo leo mchana (Jumanne, Februari 24, 2015) wakati akizungumza na viongozi mbalimbali na wananchi waliofika kushuhudia uzinduzi huo uliofanyika kwenye kata ya Lumumba, Halmashauri ya Mji wa Makambako, mkoani Njombe. 
 “Ninawasihi viongozi wa siasa tuwahimize wanachama wetu waende kujiandikisha kwa wingi. Tuache kauli za kukatisha tamaa, tuache kauli za kejeli sababu zoezi hili ni jema na lina nia ya kuwawezesha Watanzania wote kutumia haki yao ya kupiga kura,” alisema. 
 Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania wenye vitambulisho vya uchaguzi vya zamani na wale wasio na vitambulisho wajitokeze kwa wingi kushiriki zoezi hilo. 
 “Wale waliokwishafikisha miaka 18, na wale ambao watatimiza miaka 18 ifikapo Oktoba, mwaka huu wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa sababu wasipofanya hivyo hawataweza kupiga kura kama hawatajiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” aliongeza. 
 Akiwa uwanjani hapo, Waziri Mkuu alishuhudia uandikishaji wa wakazi watatu wa kata hiyo ambapo zoezi zima lilidumu kati ya dakika tatu na dakika tano. Kisha alikabidhi kadi kwa mpigakura wa kwanza kuandikishwa ambaye alitumia dakika tatu kamili. 
 Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva kwamba zoezi la uandikishaji lililoanza jana katika mji wa Makambako lilizidi matarajio ya Tume ya kuandikisha wapigakura 1,850. “Nimefarijika sana na taarifa ya Mwenyekiti... Mlianza na kata tisa zenye vituo 54 na mlitarajia kuandikisha watu 1,850 lakini badala yake mmepata watu 3,014. Hili limenipa faraja sana. Ninawapongeza sana kwa hatua hiyo,” alisema. 
 Mapema, akitoa taarifa kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu kufanya uzinduzi huo, Jaji Lubuva alisema ana imani wadau mbalimbali wataendelea kuhamasisha wananchi washiriki zoezi la uboreshaji daftari la wapiga kura. 
Alisema uboreshaji wa daftari hilo utafanyika kikanda na kwamba wamepanga kutumia siku saba kwa kila kituo huku akisisitiza kwamba hakuna mtu atakayebakizwa bila kuandikishwa wakati ameshafika kituoni. 
 Aliwataka watu wanaokwenda kujiandikisha wawe na vitambulisho vyao vya zamani vilivyotolewa na Tume ya taifa ya Uchaguzi kwani tayari vina taarifa zao kwa hiyo vitapunguza muda wa mtu kuandikishwa. 
“Kadi za Tume (NEC) au za NIDA kwa wale wachache ambao wanazo, wakija nazo zitapunguza muda wa uandikishai sababu zina taarifa kwenye kanzidata,” alisema. Akitoa ufafanuzi kuhusu mfumo wa uandikishaji wa BVR, Jaji Lubuva alisema mfumo huo siyo sawa na mfumo wa upigaji kura wa kielektroniki (e-voting) kama ambavyo wengi wanadai bali mfumo huo unafanya kazi kwa kutumia alama muhimu za mpigakura. 
 “Mfumo huu unatumia alama zaidi kwanza ikiwa ni picha na zaidi ni macho ya mhusika, pili ni alama za vidole na tatu ni saini ya mhusika. Mfumo huu unaweza pia kuchukua alama za mtu mwenye ulemavu wa kuona ama ulemavu wa mikono,” alisema. 
 Alisema uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ni hatua ya kisheria na kwamba Tume itajitahidi kuhakikisha inafuata hatua zote wakati wa zoezi hilo. 
 Waziri Mkuu ameondoka Makambako na anaelekea Mbeya kuanza ziara ya kikazi ya siku sita kukagua shughuli za maendeleo katika mkoa huo.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizindua  Uborereshaji wa Daftari kla Kudumu la Wapigakura  katika mji mdogo wa Makambako Februari 24, 2015.Kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva na Katikati ni Katibu wa Tume hiyo, Ndugu Malaba. 
   Waziri Mkuu Mizengo Pinda   na Naibu Katibu Mkuu  ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa CHADEMA  Mhe John 
 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Mwenyekititi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva (kushpoto) , Naibu Katibu Mkuu  na Katibu Mwenezi wa CHADEMA, John Mnyika (kulia), Yusufu Mbungiro ambaye ni Afisa Uchaguzi na Mafunzo taifa wa Chama cha CUF (wapili kushoto) na Allan Bujo ambaye ni Mkuu wa Ulinzi wa CHADEMA baada ya kuzinua Uborereshaji wa Daftari

  Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitazama kazi ya uandiskishaji wapiga kura baada ya ya kuzinua Uborereshaji wa Daftari kla Kudumu la Wapigakura  katika mji mdogo wa Makambako Februari 24, 2015.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...