Na Veronica Simba

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene amefanya ziara mkoani Lindi na Mtwara mwanzoni mwa wiki kukagua miradi mbalimbali iliyo chini ya Wizara yake ambapo aliahidi huduma za umeme na maji kwa wananchi mbalimbali.

Akiwa Madimba mkoani Mtwara, baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa mtambo wa kuchakata gesi, Waziri Simbachawene alimwagiza Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Bomba la gesi, Mhandisi Kapuulya Musomba kutoa huduma ya maji safi kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo.

“Kutokana na taarifa yenu, mtakuwa na hifadhi ya maji ya kutosha hapa. Pamoja na matumizi yenu mbalimbali, hakikisheni mnatoa huduma ya maji kwa wananchi wanaozunguka mtambo,” alisema Waziri. Vilevile, Waziri Simbachawene alitoa ahadi ya umeme kwa Kijiji cha Luvula kilichoko Msimbati. Alisema Kijiji hicho na vingine 15 vilivyo jirani na Kiwanda cha kufua umeme cha Mnazibay, vitapatiwa umeme kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu.

“Tunaendelea na zoezi la kusambaza umeme nchi nzima. Lengo letu ni kuhakikisha idadi ya watanzania wanaopata umeme inaongezeka zaidi na zaidi ili kuwezesha lengo la nchi yetu kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kama dira ya maendeleo inavyoonesha,” alisema.

Ziara hiyo ya Waziri Simbachawene, ni ya kwanza kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara tangu aliposhika wadhifa wa Uwaziri wa Nishati na Madini, Januari mwaka huu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda (aliyesimama), akiwasilisha taarifa fupi ya hali ya mmomonyoko wa ardhi uliosababisha mazingira ya hatari kwa Kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Maurel & Prom Tanzania (M&P), kilichopo Mnazi Bay – Mtwara. Wanaosikiliza ni Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (wa tatu kutoka Kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu (katikati), na baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Nishati na Madini walioongozana na Waziri.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, akikagua sehemu ya Mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Madimba – Mtwara wakati wa ziara aliyoifanya mwanzoni mwa wiki mkoani humo.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (wa pili kutoka Kulia) akikagua nyumba za wafanyakazi wa Mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Madimba – Mtwara. Pamoja naye ni Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Bomba la gesi, Mhandisi Kapuulya Musomba (Kushoto – sambamba na Waziri) na Mkuu wa Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud (Kulia kwa Waziri.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...