Vichwa viwili kati ya vichwa 13 vya treni vilivyonunuliwa na TRL
Machi 21, 2015 tumeshuhudia tukio muhimu sana
kwa TRL kupokea sehemu ya vichwa vipya vya treni vilivyoagizwa kutoka nje ya
Nchi. Tumepokea vichwa viwili (2) kati
ya vichwa kumi na tatu (13) vya treni vilivyonunuliwa na TRL kupitia bajeti ya
Serikali.
Vichwa hivi vimetengenezwa kupitia mkataba
kati ya TRL na Kampuni ya EMD ya Marekani.
Utengenezaji wa vichwa hivi vya treni umefanyika na Kampuni ya DCD ya
Afrika Kusini.
Ununuzi wa vichwa kumi na tatu (13) vya treni
umegharimu jumla ya Shilingi Bilioni 70.9 ambazo zote zimeshalipwa.
Hivi vichwa 13 vipya vinategemewa kupokelewa
na TRL katika awamu tatu. Awamu ya kwanza ni hii tulioshuhudia Machi 21, 2015
ambapo tulipokea vichwa viwili. Awamu ya pili itahusu kupokea vichwa vitano (5)
ambavyo vinategemewa kuwasili Mwezi Aprili, 2015. Awamu ya tatu itahusu kupokea
vichwa vingine sita ambavyo vinategemewa kuwasili mwezi Juni, 2015.
Vichwa hivi vipya vya treni vimetengenezwa
kwa kutumia tekinologia ya kisasa ya kielekroniki zaidi, na vina uwezo zaidi wa
kubeba mizigo ikilinganishwa na vichwa vya zamani. Kichwa kimoja kipya kina uwezo wa kusafirisha
tani 32,500 kwa mwaka, ukilingalinisha na tani 25,000 kwa mwaka
zinazosafirishwa na kichwa cha zamani. Ina maana kwamba kupatikana kwa hivi
vichwa vipya kutaongeza ufanisi katika utendaji kazi wa TRL. Vile vile kuwasili kwa vichwa hivi
kutaiwezesha TRL kuendesha treni za abiria mara tatu kwa wiki kutoka mara mbili
kwa wiki hivi sasa. Treni ya tatu kwa wiki itaanza safari zake tarehe 1/4/2015.
Mradi huu wa kununua vichwa 13 vipya vya
treni ni sehemu tu ya mpango kabambe wa Serikali wa kuifufua na kuiimarisha TRL
chini ya mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Mpango wa BRN kwa TRL umelenga kuiwezesha
Kampuni kiutendaji ili iweze kusafirisha tani milioni 3.0 kwa mwaka ifikapo
mwaka 2016 kutoka tani 200,000 zilizosafirishwa mwaka 2014 kupitia reli ya
kati.
Tayari tumeshuhudia hapo nyuma kupokelewa kwa
vitendea kazi mbali mbali ambavyo vimeainishwa katika mpango huu. Vitendea kazi ambavyo tayari vimepokelewa ni
pamoja na:
1. Mabehewa 25 ya
kubebea kokoto (BHBs)
2. Mabehewa 100 kati ya
274 ya kichele (CLBs)
3. Mabehewa 50 ya kubeba
makasha (CCBs)
4. Mabehewa 22 ya abiria
5. Mabehewa 17 kati ya
34 ya breki (BVBs)
6. Mtambo wa kunyanyulia
mabehewa (Breakdown crane)
7. Mtambo wa kushindilia
kokoto (Tamping Machine)
Kupatikana
kwa vitendea kazi hivi pamoja na vingine vitakavyo endelea kupokelewa
vitaiwesha TRL kusafirisha mizigo mingi zaidi na abiria wengi zaidi hatimaye
kuifanya Kampuni kujiendesha kibiashara na kwa faida na kuacha kuwa tegemezi
kwa Serikali.
Imetolewa na Afisi ya
Uhusiano kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TRL
Mhandisi Kipallo Aman
Kisamfu
Dar es Salaam,
Machi 23, 2015
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...