Na. Johary Kachwamba-MAELEZO, DODOMA
SERIKALI imeweza kushawishi mashirika ya kimataifa ya ndege kuongeza idadi ya safari pamoja na kiwango cha mzigo kinachosafirishwa kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi, ikiwemo bidhaa za matunda.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Janet Mbene alibainisha hayo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Muhammad Sanya, Mbunge wa Mji Mkongwe aliyehoji mpango wa Serikali katika kutafuta soko la matunda nje ya nchi.
Mhe. Mbene alisema TanTrade kwa kushirikiana na Chama cha Wazalishaji Maembe (AMAGRO) inaratibu mpango wa kutoa mafunzo ya uzalishaji bora, ufungashaji na kujenga kituo cha kuchambua na kupanga ubora wa maembe ili kuuzwa kwenye soko la kimataifa.
Aidha kampuni ya AMAGRO inaendelea kuhamasisha kilimo cha maembe aina ya tommy na alphonso ili kuuza soko la nje.
“mkoani Tanga tumeanzisha program ya Muunganisho wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) katika vijiji 9 ili kuzalisha machungwa yasiyo mbegu kwa matumizi ya ndani na soko la nje ” alisema Mhe. Mbene
Tayari kampuni ya Africado inayozalisha maparachichi Wilayani Hai na Kampuni ya Rungwe Avocado ambapo yote yanawakilisha wakulima wadogo, yanazalisha na kuuza maparachichi soko la nje ya nchi.
Aidha Mhe. Mbene alisema Serikali imeanzisha kampuni ya GS1 Tanzania inayoratibu mfumo wa ufuatiliaji wa mnyororo wa bidhaa ambao ni msingi mkubwa katika kupata soko la bidhaa yoyote nje ya nchi.
“Serikali inaendelea kutangaza bidhaa za Tanzania kupitia maonesho ya Biashara ya ndani, kikanda na kimataifa” aliongezea Mhe. Mbene
Mkakati wa Mauzo ya Nje (National Export Strategy) wa Mwaka 2009 ulibainisha mikakati ya kuongeza mauzo ya matunda, maua na mbogamboga. Kutokana na hali hii thamani ya mauzo ya matunda nje imeongezeka kutoka Dola za kimarekani 7,440,290 mwaka 2010 hadi Dola za kimarekani 32,116,895.22 mwaka 2013.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...