Na Ally Rashid Dilunga, London
Katika kukamilisha mojawapo ya malengo ya
ziara yake ya kikazi hapa Uingereza, Naibu waziri wa viwanda na biashara
Mheshimiwa Janet mbene, amemalizia ziara yake ya wiki moja nchini Uingereza kwa
kukutanishwa na baadhi ya wafanyabiashara wa Kitanzania hapa Ubalozini jijini
London.
Ametumia fursa hiyo kuwafahamisha hatua
zinazochukuliwa na Serikali kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na pia
kuwataarifu juu ya fursa za kibiashara zilizoko katika sekta mbalimbali nchini
Tanzania na kuwahamasisha kuzichangamkia fursa hizo na wasiwe ni wenye
kuwaachia tu wanufaike nazo wageni.
Amewaambia kuwa kuna njia nyingi za
kujishughulisha kibiashara, kuanzia kwao wenyewe kuwa ni sehemu ya masoko kwa
kuwa waagizaji na wasambazaji wa bidhaa za Kitanzania, au kwa kushawishi
wawekezaji kuja kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini au kuingia nao ubia.
Hata hivyo nao walimlalamikia Mheshimiwa
Naibu Waziri juu ya ukosefu wa taarifa za biashara juu ya miradi ya uwekezaji
nchini, ambapo naye amekiri upungufu huo na kwamba ushauri wao ameuzingatia.
Tangu alipowasili nchini Uingereza,
Mheshimiwa Mbene alikutanishwa na wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali
kupitia Vyama vyao vya kibiashara na pia alikutana na baadhi ya wafanyabiashara
na wawekezaji binafsi na kufanya nao mazungumzo yenye lengo la kuwekeza kwenye
uongezaji thamani wa mazao au kufanya biashara hasa kwa kuvipatia masoko bidhaa
kutoka nchini Tanzania.
Viongozi wa vyama vya kibiashara na baadhi
ya wanachama wao aliokutanishwa nao ni wa Eastern Africa Association (EAA),
Business Council for Africa (BCA) na UK-Tanzania Business Group.
Mheshimiwa Janet Mbene pia alikutanishwa na
mshauri wa Serikali ya Uingereza juu ya masuala ya biashara kwa Tanzania, Lord Clive Hollick na watendaji wengine wa Idara ya
uhamasishaji uwekezaji na Biashara (UKTI), ambapo alielezwa baadhi ya
changamoto wanazokumbana nazo wawekezaji nchini Tanzania. Mheshimiwa Mbene alitumia
fursa hiyo kuwapa ushauri anaoamini utasaidia kupatikana kwa
ufumbuzi wa changamoto hizo na hasa baada ya mifumo ya utendaji kazi serikalini
kurekebishwa kupitia Mpango maalum wa Matokeo Makubwa sasa (BRN).
Katika siku ya tatu ya ziara yake, mheshimiwa
Mbene alitembelea Ofisi za Ubalozi na kukutana na watumishi wa Ubalozi na
baadaye kukitembelea Kituo cha Biashara na kupata maelezo juu ya shughuli zake
na changamoto zake.
Pia kutokana na ziara yake na kuongea na
wafanyabiashara mbalimbali, Mheshimiwa Mbene amegundua kuwa Kituo kinafanya
kazi kwa karibu sana na wafanyabiashara wa Ulaya, hivyo Serikali inatakiwa
kukiongezea Kituo nguvu zaidi ili kiweze kutekeleza majukumu yake mengi kwa
ufanisi zaidi na kuendelea kutoa mchango wake mkubwa katika kufanikisha malengo
ya kiuchumi ya Taifa, kama ilivyokusudiwa.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Tanzania, Mheshimiwa Janeth Mbene(kulia), akiongea na Mwakilishi wa Serikali ya Uingereza katika masuala ya Biashara na Uwekezaji nchini Tanzania, Lord Clive Hollick, walipokutana kuzungumzia masuala ya Biashara ya kati ya nchi mbili ya Tanzania na Uingereza na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Uingereza kusaidia wawekezaji wa Kiingereza kuwekeza Tanzania.
Mheshimiwa Janeth Mbene, akiongeza na Wawekezaji na Wafanyabiashara wa Kiingereza alipokutana nao kwa mwaliko wa Kituo cha Biashara cha Tanzania, London na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa East African Association. Mheshimiwa Naibu Waziri alikutana na Wafanyabiashara hao kwa lengo la kuwashawishi kuja kuwekeza nchini Tanzania
Mheshimiwa Waziri Janeth Mbene(kulia), alipokutana na Mwakilishi wa Serikali ya Uingereza na Chama cha Wafanyabiashara na Wawekezaji wa nchini Uingereza (UKTI) (kati mwa picha), kushoto ni Mkurugenzi wa Kituo cha Biashara cha Tanzania nchini Uingereza, Bwana Yusuf Kashangwa.
Wawakilishi wa Jumuiya za Wafanyabiashara na Wanachama wa chama cha Wafanyabiashara wa Tanzania nchini Uingereza (Tanzania Business Group) wakimsikiliza Naibu Waziri wa Viwanda, Mheshimiwa Janeth Mbene, alipokutana na kuzungumza nao siku ya Ijumaa tarehe 28 Februari 2015, mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, London. Mheshimiwa Waziri alikutana nao kuzungumzia hali ya Siasa na Uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Mheshimiwa Waziri aliwakumbusha Wafanyabiashara hao kutumia fursa zilizopo na kuwekeza nyumbani Tanzania, kwa lengo la kuongeza ajira na kuinua uchumi wa nchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...