Msimamizi wa mradi wa FAO kijiji cha Kiroka mkoani Morogoro, Ajuaye Sigalla, akitoa muhtasari wa maendeleo ya mradi FAO unaotekelezwa na wanakikundi wa Umoja wa Wakulima Kiroka (UWAKI) mbele ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kushoto) na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Filiberto Sebregondi walipofanya ziara ya kugagua miradi yao ya maendeleo mkoani Morogoro.(Picha na Zainul Mzige)
Na Mwandishi wetu, Morogoro
BALOZI wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Filiberto Sebregondi ametembelea skimu ya umwagiliaji ya Kiroka na kusema kwamba atahakikisha kwamba kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwamo serikali wataendelea kusaidia wananchi kujiinua kiuchumi.
Akiwa katika skimu hiyo inayosaidiwa na Shirika la Chakula duniani (FAO) ametaka miradi ya maendeleo nchini kutowaacha nyuma wanawake na watoto kwani wao ndio msingi wa maendeleo ya kijamii kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa.
Balozi huyo ambaye anatarajiwa kurejea Ulaya mwaka huu baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini amesema kwamba kuwapo kwa asilimia 60 ya wafaidika na mradi huo wa Mpunga kuwa wanawake kumesaidia sana kuamsha maendeleo ambayo yanatakiwa kuendelea kusimamiwa.
"Wanawake wamefanikiwa kupeleka watoto wao shuleni. kuwapatia chakula kinachostahiki na kupata kipato na katika hili ni vyema wasiachwe nyuma kimaendeleo" alisema balozi huyo.
Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Filiberto Sebregondi akizungumza na wanakikundi wa Umoja wa Wakulima Kiroka (UWAKI) wanaofadhiliwa na FAO wakati wa ziara ya kutembelea miradi inayofadhiliwa na wadau wa maendeleo ambapo mradi wa Kiroka unafadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la FAO huku mradi wa makazi mapya kwa waathirika wa mafuriko Kilosa ukifadhiwa na Ubalozi wa Umoja wa Ulaya. Kushoto kwake ni Msimamizi wa mradi wa FAO kijiji cha Kiroka mkoani Morogoro, Ajuaye Sigalla.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...