Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli ametangaza kutobomolewa nyumba zilizopo kando kando ya  barabara ya Mwanga-Kikweni/Vuchama-hadi Lomwe km 40.6 na kusema kuwa barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami kwa kutumia upana wake uliopo hivi sasa.
Dkt. Magufuli alitoa kauli hiyo ya faraja kwa wakazi wa Kikweni Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro kabla ya kuweka jiwe la msingi katika barabara ya Mwanga-Kikweni/Vuchama-Usangi hadi Lomwe(km 40) itakayojengwa kwa kiwango cha lami hivi karibuni.
Waziri wa Ujenzi amechukua uamuzi huo kutokana na maeneo mengi ya milimani ambapo barabara hiyo inapita kuwa na mashamba ya watu tofauti na sehemu nyingine.
“Nikiwa kama Waziri wa ujenzi katika maeneo haya ya milima sitatumia sheria ya mita 30 kila upande katika ujenzi wa barabara hii ili nyumba na mashamba ya wakazi wa huku yasiathirike”
Dkt. Magufuli aliongeza kuwa ujenzi wa Barabara una sheria zake ndio maana ameamua kutumia sheria ya barabara  namba 13 ya mwaka 2007 kifungu cha 13 na 20 kinachompa mamlaka kupunguza upana wa barabara
Aidha, Waziri Magufuli aliwatoa hofu wakazi wote waliowekewa alama ya X katika nyumba zao na kuwataka kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwasababu nyumba hizo hazitabomolewa.
Katika hatua nyingine Dkt. Magufuli aliwataka watu wote waliojenga vibanda karibu na barabara ya zamani waanze kuondoka mapema kabla ya ujenzi wa barabara hiyo kuanza hivi karibuni.
“Nawaomba wote mlioweka vibanda karibu na barabara mtoe kwa hiari yenu ili tutengeneze barabara hii bila vikwazo na kwa haraka tofauti na awali ambapo tulikuwa tunatangaza zabuni kwa kilomita chache” alisisitiza Waziri Magufuli
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama amemshukuru Waziri Magufuli kwa hatua yake hiyo na kusema kuwa kufunguka kwa barabara hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wilaya ya Mwanga na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.
“Wilaya yetu hii inapakana na nchi jirani hivyo hata kiusalama ni vizuri barabara hii ikajengwa kwa lami ili irahisishe mawasiliano kwa haraka zaidi katika Wilaya yetu hii” alisema Mkuu wa Mkoa
Naye Mbunge wa Mwanga ambaye pia ni Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe ameishukuru Serikali na kusema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutawaondolea kero kubwa ya usafiri wananchi wa Usangi na mwanga na kuwasaidia kufanya biashara kwa urahisi zaidi tofauti na awali.
“Kukamilika kwa barabara hii kutasaidia kuinua uchumi mkubwa uliopo huku Usangi tofauti na hali iliyopo sasa” Alisema Profesa Maghembe.

 Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli katikati akiweka jiwe na msingi kuashiria kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Mwanga-Kikweni-Vuchama-Usangi-Lomwe yenye urefu wa kilomita 40. Kulia kwake ni Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Mwanga Profesa Jumanne Maghembe, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama pamoja na viongozi wengine wa Wilaya ya Mwanga.
 Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli kushoto akizungumza jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Musa Iyombe kabla ya kuweka jiwe la msingi katika barabara ya Mwanga-Kikweni-Vuchama-Usangi-Lomwe yenye urefu wa kilomita 40.6. Katikati ni Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Mwanga Profesa Jumanne Maghembe.
 Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama wakicheza ngoma na kikundi cha ngoma za asili Kikweni kabla ya uzinduzi wa barabara ya Mwanga-Kikweni-Vuchama-Usangi-Lomwe yenye urefu wa kilomita 40.
 . Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli akipiga ngoma na kikundi cha ngoma cha Msanja group kabla ya kuhutubia mamia ya wakazi wa Usangi kuhusu ujenzi wa barabara ya Kikweni-Usangi-Lomwe ambayo itaanza kujengwa hivi karibuni.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...