Mwakilishi wa Kudumu wa  Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi akibadilishana  mawazo na  Bw. B. Lynn Pascoe  ambaye ni kati ya wajumbe 14 wa Tume Huru iliyoundwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  kufanya tathmini kuhusu hali ya sasa ya Operesheni za Ulinzi wa Amani pamoja na  Misheni Maalum za Kisiasa. Tume hiyo huru iliyoteuliwa  mwishoni mwa mwaka jana imekwisha anza kazi.

 Jana ( Jumatano ) Baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo akiwamo Bw. Pascoe walikutana katika  majadiliano yasiyorasmi na   Wawakilishi wa  Kamati Maalum ya  Nne ya Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa na kubadilishana  mawazo kuhusu masuala  ya jumla yahusuyo Misheni Maalum za Kisiasa. Mkutano huo uliandaliwa na  Idara ya Siasa ya Umoja wa Mataifa.

Akichangia  majadiliano hayo,  Balozi Manongi, amesema kwamba Misheni  Maalum za Kisiasa,  pamoja na umuhimu wake na mchango wake katika mustakabali wa amani na  usalama,  lakini  ni misheni ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na  nchi wanachama,  hasa kutokana na ukweli kwamba uundwaji wake hauko wazi, si shirikishi wala  jumuishi.

 Kutokana na  mazingira hayo,  Balozi Manongi ameishuri Tume hiyo Huru kuliangalia  kwa mapana suala la Misheni Maalum za Kisiasa ikiwa ni pamoja na  muundo wa  uundwaji wake na pia kuboresha uwazi, uwajibikaji  na  uwakilishi utakaozingatia uwakilishi   jumuishi wa kila  kanda.

Kama ilivyokuwa kwa wazungumzaji wengi,  Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa  ameelezea matumaini yake kwamba Taarifa itakayoandaliwa na Tume hiyo  Huru itazingatia michango na maoni ya  nchi wanachama kwa lengo la  kuboresha Operesheni za Ulinzi wa Amani ambazo  kwa sasa zinakabiliwa na changamoto nyingi na vilevile kuboresha utendaji wa Misheni Maalum za Kisiasa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...