Mkongwe Dr Mulatu akijituma


Dr Mulatu akikong'ori vigoma vyake

Dr Mulatu na Leo wakishebedue

Ziara ya Swahili Blues Band mjini Addis Ababa ilimalizika rasmi siku ya Jumamosi ya tarehe 11 April 2015 katika klabu mpya na maarufu ya African Jazz Village.

Kama ilivyo kawaida, shoo ilianza rasmi saa tatu na nusu usiku pale Swahili Blues Band ilipopanda jukwaani na kuanza kuporomosha nyimbo zao mfululizo. Waliendelea na midundo hiyo kwa muda wa saa moja na ilipotimia saa nne na nusu ndipo Leo Mkanyia alipowaita stejini mpiga zeze la kihabeshi (krar) maarufu wa Ethiopia anayejulikana kwa jina la Mesele na gwiji mwenyewe wa miondoko ya Ethio Jazz Dr Mulatu Astakte.

Hapo ndipo lile vuguvugu maalumu linalojulikana kama Ethio- Tanzanian Fusion lilipoendelea kushika kasi. Bendi ilipiga nyimbo zao nane mfululizo huku vionjo vya kihabeshi vikiingizwa ndani kupitia kwenye krar, vigoma vidogo na vibraphone vilivyokuwa vikicharazwa kwa umahiri mkubwa na Dr Mulatu Astakte. Nyimbo zilizopigwa zilikuwa ni Aichelelo, Seychelles, Wazazi Wangu, Afrika, Dar es Salaam, Sawa Saware, Haki na Shikandambwe. Shoo hiyo pia ilipambwa vilivyo na wasichana wawili wanenguaji wa Kihabeshi ambao walibamba vizuri kwa kucheza kihabeshi midundo ya kiswahili.


Jioni hiyo pia ilikuwa maalumu kwa wageni waalikwa kutoka balozi mbalimbali ambao walifika kuja kuunga mkono vugu vugu la kutambulisha muziki wa Afrika Mashariki kimataifa. Wageni hao maalumu walijumuisha mawaziri waandamizi wawili kutoka serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mabalozi kutoka nchi za Senegal, Ubelgiji, Mexico, Togo, Uturuki, Georgia, Uholanzi na Afrika ya Kusini. Vilevile walihudhuria maofisa waandamizi kutoka ubalozi wa Marekani, Ufaransa na Umoja wa Afrika yaani AU.

Ethio- Tanzanian Fusion iliendelea kuwashikilia vilivyo waalikwa hao hadi saa tano na dakika arobaini na tano pale Leo Mkanyia alipowatambulisha wanamuziki wote walioshiriki katika shoo hiyo kabambe na maalumu kabisa. Mara baada ya Leo kutambulisha wanamuziki, Dr Mulatu Astakte alichukua kipaza sauti na kuwashukuru wote waliohudhuria na kuelezea umuhimu wa vuguvugu hili linalojumuisha muziki wa kweli kutoka Afrika ya Mashariki. Aliendelea kwa kutoa rai kwa wadau wote wa kimataifa kutoa ushirikiano kwa juhudi za pamoja zakuufanya muziki wa Afrika ya Mashariki ufike mbali na mipaka ya nchi hizo kama ilivyo kwa pande nyingine za Afrika kama vile Kusini, Magharibi na Kaskazini. Vile vile alitoa pongezi kwa Swahili Blues Band kwa kuwa na ushupavu wa kuthubutu kupiga muziki usiotharika na utamaduni kutoka sehemu nyingine tofauti na Afrika Mashariki. Aliendelea kuwasisitiza kuwa wako kwenye njia sahihi kwa kupiga muziki wenye mizizi ya kiutamuduni ya Kiswahili yenye ladha na mchanganuo wa kimataifa.

Shoo hiyo maalumu ilimalizika rasmi saa sita kasoro dakika tano kwa tukio la kihistoria pale mpiga tumba na Marimba wa Bendi Juma Setumbi alipompa zawadi ya Marimba Bendi Dr Mulatu Astakte. Juma Setumbi alidai kuwa lengo la kumpa zawadi ya Marimba Dr Mulatu ni kutambua juhudi zake za zaidi ya miaka 50 katika muziki wa ki Ethiopia. Vile vile ni kumshukuru kwa kutoa wazo na kuanzisha Ethio-Tanzanian Fusion pamoja na kuonyesha ushirikiano wa hali ya juu alioonyesha kwa Bendi ndogo kama hii wakati yeye ni mwanamuziki mkubwa sana wa kimataifa.

Lilikuwa ni tukio kubwa na la kihistoria ukizingatia kuwa Dr Mulatu hajazoea kupokea bali yeye siku zote amekuwa mtu wa kutoa tu. Alimshukuru sana Juma kwa zawadi hiyo na kuahidi kuendeleza ushirikiano huu muhimu sana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...