Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene amesema kuwa Shirika la
Umeme Nchini (Tanesco) lina mpango wa kufunga mita za LUKU katika ofisi za taasisi
zote za serikali kama moja ya mikakati yake katika ukusanyaji wa mapato.
Simbachawene aliyasema hayo wakati wa kikao chake na Balozi wa Marekani Nchini,
Mark Childress aliyemtembelea ofisini kwake lengo likiwa ni kujadili hatua iliyofikiwa ya
utekelezaji wa mpango wa kuboresha sekta ndogo ya umeme na miradi ya Mfuko wa
Changamoto za Milenia (MCC).
Alisema kuwa kama mkakati wa kuhakikisha kuwa shirika la Tanesco halijiendeshi
kihasara, shirika hilo limeweka mkakati wa ukusanyaji wa mapato, moja ya mkakati
ikiwa ni kufunga mita za Luku kwenye Taasisi za Serikali, Binafsi na wateja wa
kawaida.
“Tunaamini shirika likitekeleza mkakati huo, litapunguza hasara na kuwa tegemezi
kwenye serikali kupitia ruzuku.” Alisema Simbachawene.
Alisema pia Tanesco itaingia mkataba na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) kwa
ajili ya ukusanyaji wa madeni yake ya nyuma na kuendelea kulipia ankara zake za kila
mwezi.
Akizungumzia hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa miradi ya MCC Awamu ya Pili ,
Simbachawene alisema kuwa kazi ya uandaaji wa miradi imekamilika na kuwasilishwa
katika Bodi ya MCC nchini Marekani kwa ajili ya kupata idhini ya kufadhili miradi
Alitaja mikoa itakayofaidika na miradi ya MCC Awamu ya Pili kuwa ni pamoja na
Pwani, Tabora, Shinyanga na Morogoro pamoja na kuboresha utendaji kazi wa
Tanesco.
Wakati huohuo Balozi wa Marekani Nchini, Mark Childress alisema kuwa
amefurahishwa na hatua ya utekelezaji wa miradi ya MCC Awamu ya Pili na kusisitiza
kuwa Marekani ipo tayari kushirikiana na nchi ya Tanzania kupitia miradi ya umeme
ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata umeme wa uhakika ambao una mchango
mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Balozi wa Marekani Nchini, Mark Childress (kushoto) akizungumza na Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene (kulia) kwenye Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini .
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia) akiagana na Balozi wa Marekani Nchini, Mark Childress (kushoto) mara baada ya mazungumzo kwenye ofisi za Wizara ya Nishati na Madini.
Hii itasaidia kubajeti fungu la kulipia huduma ya umeme.
ReplyDelete