Mchapishaji wa Kitabu kipya chenye historia ya nchi tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964,Javed Jafferji (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya Uzinduzi wa Kitabu hicho   April 24 mwaka huu katika Hoteli ya Serena  jijini Dar es Salaam,Mhariri Mkuu wa Kitabu Simai Mohammed.
Mhariri Mkuu wa Kitabu kipya chenye historia ya nchi tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, Simai Mohammed  akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya Uzinduzi wa Kitabu hicho April 24 katika Hoteli ya Serena  jijini Dar es Salaam,Mchapishaji wa Kitabu kipya aved Jafferji. (Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya Jamii)

Na Bakari Issa,Globu ya Jamii
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Jakaya M.Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Kitabu kipya chenye historia ya nchi tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.

Kitabu hicho chenye kurasa 444 kinaelezea historia ya nyuma ya kisiwa cha Zanzibar pamoja na Tanzania Bara na safari ya kisiasa tangu mwaka 1964,kinatarajiwa kuzinduliwa kesho April 24 katika Hotel ya Serena,saa 12 jioni  jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Wandishi wa Habari,Mhariri Mkuu wa Kitabu hicho, Simai Mohammed amesema kitabu hicho kinazungumzia undugu ulioko kati ya kisiwa cha Zanzibar pamoja na Tanzania Bara,pamoja na matukio muhimu ambayo yamewagusa Watanzania kama Vita vya Kagera pamoja na kifo cha Mwalimu Julius K.Nyerere.

Mchapishaji wa Kitabu hicho,Javed Jafferji amesema kitabu hicho kimechukua miezi  17 kuchapishwa,vilevile kimeelezea historia fupi ya Rais wa Tanzania, Dkt.Jakaya M.Kikwete  pamoja na wa Tanzania visiwani,Dkt.Ali Mohammed Shein.

Jafferji aliongeza kuwa  amefurahishwa sana na Kitabu hicho kutokana na kuelezea historia ya nchi yetu pamoja na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Ankal,

    Shukrani kwa taarifa hii murua. Ndugu Javed Jafferji ni mpiga picha maarufu duniani, ambaye amekuwa akitangaza Tanzania kwa umahiri mkubwa njia ya vitabu vyake vya picha. Picha zake zimetokea pia katika majarida maarufu ulimwenguni.

    Sina shaka kuwa kitabu chake hiki kipya ni hazina juu ya hazina. Kinachosikitisha ni ukosefu wa utamaduni wa kuvinunua na kuvisoma vitabu katika jamii yetu ya Tanzania.

    Tumeshuhudia uzinduzi wa vitabu tena na tena. Mifano ni kitabu cha Mzee Edwin Mtei, kitabu cha Mzee Rashidi Kawawa (Simba wa Vita), kitabu cha Profesa Julius Nyang'oro juu ya JK. Lakini baada ya uzinduzi, vitabu hivi havisikiki tena.

    Ni tofauti na nchi kama Kenya, ambako hata magazeti yao huwa ni uwanja wa mijadala ya vitabu. Magazeti yetu Tanzania, na vyombo vya habari kwa ujumla, vina ajenda zao, lakini si vitabu. Ni dalili nyingine ya kuanguka kwa elimu. Tujirekebishe.

    ReplyDelete
  2. The mdudu, hivi kweli penye njaa ya kufa mtu panasomeka? na wewe mdau hapo juu hamia Kenya tuachie Tanzania yetu kama ilivyo maana mifano yako haina nyuma wala mbele hivi ushafika Kenya uwone wananchi wanavyo taabika? wakenya wengi wao wanasoma magazeti na vitabu mchana ila jioni ikifika majonzi maana hawana pa kulala sasa hii akili au matokeo?

    ReplyDelete
  3. Anonymous, tangu tulipopata Uhuru, Mwalimu Nyerere alituambia kuwa tuna maadui watatu ambao tunatakiwa kupambana nao: ujinga, umaskini, na maradhi. Wewe unaukingia kifua ujinga.

    Kenya ninaifahamu kutosha, nimepita sehemu kama Nairobi, Kisumu, Mombasa, Witu, na Lamu. Sikuwa napita kama msafiri, bali katika shughuli za utafiti. WaKenya nawaona walivyo huku ughaibuni, Marekani.

    Kuanzia nchini kwao hadi huku ughaibuni, ni watu wanaothamini na kuvisoma vitabu, tofauti na wa-Tanzania. Mimi ni mwandishi wa vitabu na nimeshudia hayo katika maonesho ya vitabu, maduka ya vitabu, na katika kufahamiana na watu Kenya na Tanzania na huku ughaibuni.

    Nimeandika mara kwa mara kuhusu hayo katika blogu yangu, na waandishi na wad au wa vitabu Tanzania wamekuwa wakilalamika kama ninavyolalamika.

    Kuhusu uwezo wa kununua vitabu nimeandika sana. Wa-Tanzania kwa ujumla wanazo hela za kununulia vitabu. Kwa sababu ya ujinga, hawaoni faida ya vitabu, bali wanatumia hela zao kwenye sherehe, ulabu, "bonanza," makamuzi, mashindano ya urembo, kabumbu na kila aina ya mambo kama hayo. Utawakuta wamefurika huko.

    Lakini linapokuja suala la vitabu, wanatoa kauli kama hii yako, kwamba mtu anayehangaikia kupata angalau mlo moja kwa siku atanunuaje au kusoma vitabu. Hoja hii inaweza kuwa na ukweli kwa baadhi ya watu, lakini huo utitiri unaoonekana kwenye makamuzi na starehe je? Hayo mamilioni ya shilingi yanayotumika kununulia bia kila siku na kila wiki nchini je?

    Mimi ni mwalimu. Siwezi kusaliti wajibu wangu wa kupambana na adui ujinga. Soma blogu yangu ya "hapakwetu" utaona ushahidi, tena na tena.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...