Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati wa Mkutano wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu upokonyaji wa silaha. wajumbe wa mkutano huo wamejadiliana pamoja na mambo mengine umuhimu wa kudhibiti matumizi ya silaya za nyukili ikiwa ni pamoja na kusambaa kwake pamoja kuanzishwa kwa Ukanda huru dhidi ya silaha hizo.
Sehemu ya wajumbe wa mkutano wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya upokonyaji wa silaha, mkutano huu unafanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Jijini New York.

Na Mwandishi Maalum, New York
Udhibiti  wa    silaha za nyukilia na tishio la   mataifa mengine  la kujilimbikiza silaha hizo limendelea kuchukua sehemu kubwa ya majadiliano katika duru za  Umoja wa Mataifa.

Kwa mara nyingine tena mataifa yanayo miliki silaha hizo yameendelea kutetea uhalali wa kuwa nazo,  huku zile ambazo hazina  hasa  nchi zinazoendelea, licha ya  kuhimiza kuhakikishiwa usalama wao,  kutaka kuanzishwa kwa kanda huru dhidi ya silaha hizo, pia zimesisitiza haki ya kufanya utafiti,  kuzalisha na kutumia nguvu za nyukilia kwa matumizi ambayo ni salama.

Kwa siku mbili mfululizo ( jumanne na jumatano) nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, wamekuwa na majadiliano ya jumla kuhusu upokonyaji wa silaha zikiwamo silaha za nyukilia, silaha ndogo  na nyepesi wakati wa Mkutano wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa  kuhusu upokonyaji wa silaha ( UNDC).

Mkutano huo ambao ulikuwa uanze  rasmi siku ya jumatatu lakini  ukashindikana  kuanza siku hiyo baada ya wajumbe kushindwa kukubaliana juu ya ajenda za mkutano .

Akiungana  na wazungumzaji  wengine, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi,  pamoja na  kutoa wito wa kuanzishwa kwa kanda huru dhidi ya silaya za nyukilia,  amesititiza udhiti wa silaha hizo kwa kile alichosema,  bila  kufanya hivyo   mataifa mengi yatajiunga katika mbio za kutaka  kujilimbikizia silaha hiyo na  hivyo kuiweka dunia katika hatari kubwa.

Balozi  Manongi, kama ilivyo kuwa kwa wasemaji wengine wengi, amesema  Tanzania  inaamini katika majadilianao ya  pamoja kupitia Umoja wa Mataifa ambao anasema ndilo eneo ambalo linaweza kuwakilisha mawazo ya wengi na hatimaye kutoka na  kauli ya pamoja kuhusu upokonyaji wa silaha za aina zote pamoja na kudhibiti usambaaji wake.

“ Wakati   tukizihimiza  nchi zenye silaha za nyukilia  kutuhakikisha  usalama wetu  na vilevile  kujizuia kutoa vitisho vya kutumia silaha hizo kwa kisingizio chochote au katika  mazingira yoyote yale. Tunaka haki ya  sisi mataifa  yanayoendelea kuwa na fursa ya kufanya utafiti, kuzalisha na kutumia nguvu za nyukilia kwa matumizi salama” akasisitiza Balozi Manongi.

Katika mchango wake,  Tanzania kupitia mwakilishi wake, imeelezea wasiwake wake kuhusu Kamisheni ya Upokonyaji  silaha ambayo   kwa miaka  kumi na tano  imeshindwa  kuwasilisha mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mapendekezo ya aina yoyote ile.

Kushindwa kwa Kamisheni hiyo kuwasilisha  mapendekezo yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kunatokana na mambo mengine kwa wajumbe wa  Kamisheni hiyo kushindwa kufikia makubaliano  yenye tija.

Na kwa sababu hiyo Tanzania imewataka wajumbe  wafikie mahali waache tofauti zao na kuonesha utashi wa kisiasa. Huku ikisisitiza kwamba  utashi   wa kisiasa  utaiepusha dunia na matumizi ya  silaha za  nyukilia, matumizi ambayo hata  Mahakama ya Kimataifa imesema  yatakuwa yanakwenda kinyume  na Katiba ya Umoja wa Mataifa.

Balozi Manongi akawaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, Tanzania  ina imani kubwa na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki kama chombo  muhimu chenye mamlaka ya  kusimamia na kudhibiti   shughuli au  program za nguvu za nyukilia zinazolenga katika matumizi salama.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...