Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuwapa kipaumbele wakulima wadogo kwa kuandika habari zao kiundani kuliko kuegemea kwa wanasiasa peke yao.

Mwenyekiti wa Mtandao wa vikundi vya wakulima nchini (Mviwata), Veronica Sophu aliyasema hayo jana mjini Morogoro kwenye kongamano la waandishi wa habari wanaoandika habari za wakulima.

Sophu ambaye alikuwa mjumbe wa Bunge maalum la Katiba (BMK) kupitia kundi la wakulima alisema wakulima nchini wanatakiwa wasikilizwe kwani wana changamoto nyingi zinazowakabili.

“Kuna changamoto ndogo kati ya waandishi wa habari na wakulima kwani vyombo vingi vya habari vimekuwa vinaegemea kwa wanasiasa na kutuacha wakulima bila kuwa na mahali pa kusemea,” alisema Sophu.

Alisema mara nyingi habari za wakulima wadogo hazipewi kipaumbele zaidi ya migogoro kati yao na wafugaji hivyo waandishi wa habari wabadilike kwa kuwatazama na wao.

“Asilimia kubwa ya watanzania ni wakulima wadogo kwani kila kwenye watu 10 kati yao nane ni wakulima hivyo wapewe kipaumbele kwani bila mkulima mdogo hatuwezi kupata chakula nchini,” alisema Sophu.

Naye, Mkurugenzi mtendaji wa Mviwata Stephen Ruvuga alisema mchango wa waandishi wa habari nchini kwa upande wa wakulima mdogo ni wa muhimu hivyo uzingatiwe.

Ruvuga alisema wakulima wadogo wanatakiwa kuungwa mkono na waandishi wa habari kwa kusemewa kwa namna nzuri zaidi kuliko kuripoti tuu habari hizo bila kuingia kwa undani.

“Wakulima wadogo wana nafasi kubwa katika kuchangia uchumi wa Taifa na jamii kwa ujumla hivyo waandishi wa habari msiangalie tabaka la juu pekee na kuacha kutoa habari za wakulima,” alisema Ruvuga.
Mwenyekiti wa Mviwata Veronika Sophu akizungumza na waandishi wa habari wanaoandika habari za wakulima (kulia) ni Mkurugenzi wa Mviwata Stephen Ruvuga na kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Mviwata Usi Haji Usi.
Waandishi wa habari kutoka mikoa mbalimbali nchini wanaoandika habari za wakulima wakifuatia kongamano la waandishi wa habari marafiki wa wakulima lililowashirikisha waandishi mbalimbali kutoka vyombo na mikoa tofauti, lililofanyika mjini Morogoro na kuandaliwa na Mviwata.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 08, 2015

    karibu kwenye tovuti ya kuwapa ushauri wa bure wakulima:

    http://ushaurikilimo.org/index.php

    https://www.facebook.com/Ict4AgriculturalExtensionServices

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...