Maisha Lab ya Uganda wametangaza
kuwa warsha yao nyingine itafanyika Zanzibar wakati wa ZIFF 2015 mwezi Julai
kuanzia tarehe 18 hadi 25. Maombi toka kwa wanaotaka kushiriki katika warsha
hii yameanza kupokewa na mwisho wa maombi ni tarehe 13 Juni.
Warsha za Maisha Lab zimekuza
vipaji vya waandishi wa filamu na wakurugenzi wa filamu wengi hapa Afrika
Mashariki. Tayari warsha hizo zimefundisha zaidi ya watu 1000 tangu Maisha Lab
ianzishwe.
Mkurugenzi wa Maisha Lab aliyeko
Kampala Uganda alisema kuwa wanataraji kutoa skolaship 60 kwa wanafunzi kwa
mwaka kwa washiriki toka nchi zote za Afrika Mashariki.
“Katika warsha zetu watu 60 (15
toka kila nchi) watachaguliwa kuhudhuria mafunzo hayo yatakayoongozwa na
wakufunzi waliobobea katika fani za uandishi wa filamu. Nia ni kuongeza ujuzi na kupanuwa wigo wa biashara ya
utengenezaji filamu hapa Afrika Mashariki.” Alisema Fibby Kioria Mkurugenzi wa
Maisha lab.
Katika kila Warsha script
zitashindanishwa na mshindi atapatiwa $5000 ili kumwezesha kutengeneza filamu
fupi katika mwaka unaofuata. Mwaka jana Nassir Qassim wa Tanzania ndiye
aliyeibuka mshindi.
Hii ni warsha ya 3 itakayofanyika
Zanzibar na ZIFF ndio mdhamini wake ili kuwapa washiriki nafasi ya kushiriki
katika tamasha na hivyo kuweza kukutana na watengeneza filamu wengine toka nje
wanaokuja kwa ZIFF. Pia wanapata nafasi ya kuangalia filamu tele zinazoonyeshwa
wakati wa Tamasha.
Lakini Mkurugenzi wa ZIFF
aliharakisha kusema kuwa anasikitishwa sana kuona kuwa washiriki toka Zanzibar
huwa wachache kila mwaka. “Tunajuwa kuwa waandishi wa filamu toka zanzibar
wanahitaji sana mafunzo haya maana yanawapa ujuzi na pia nafasi ya kujuana na
watengeneza filamu wengine wa kimataifa”, alisema Mkurugenzi huyo
Tasnia ya filamu ya Bongo Movies
imesemwa sana kwa kuwa na hadithi dhaifu kimataifa. Kwa kutumia warsha kama
hizi wadau wanaweza kukuza vipaji vyao na kufikia hadhi ya kimataifa.
ZIFF mwaka huu imejitolea
kuwasaidia wale wote ambao wangependa kutuma maombi yao ili kuwasaidia kufuata
malekezo ya usaili, kuwapa miongozo ya uandishi wa skripti na kuwaongezea
nafasi za kuchaguliwa kuhudhuria warsha hii muhimu. Wanaotaka kusaidiwa katika
hili wanatakiwa kufika ZIFF, Ngme Kongwe Zanzibar, au kutuma maombi yao ya
kusaidiwa kwa barua pepe workshop@ziff.or.tz
Wanaotaka kujua zaidi kuhusu
warsha hii waingie kwenye tovuti hii: www.maishafilmlab.org au wawasiliane na fibby@maishafilmlab.org
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...