*Aahidi kuchangia madawati 135 na viti vyake
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameahidi kuchangia madawati 135
na viti vyake kwenye shule ya msingi Kiembesamaki iliyoko wilaya ya
Magharibi mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni mwitikio wa maombi aliyopewa
na shule hiyo.
Ametoa ahadi hiyo jana (Jumamosi, Mei 2, 2015), wakati
akikabidhi msaada wa madawati 45 na viti vyake yenye thamani ya sh.
milioni 3.83/- yaliyotolewa na kampuni ya Jambo Plastics ya Dar es
Salaam ili kupunguza uhaba wa madawati katika shule za Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
“Tatizo la madawati ni la kitaifa… Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali ametuambia kwamba haya ya leo yatatosha darasa moja tu
na bado kuna mengine matatu hayana kabisa madawati. Changamoto iliyopo
hivi sasa ni kwamba haya madawati yatagawanywa vipi wakati watoto
wengine bado hawana mahali pa kukaa?” alihoji Waziri Mkuu.
“Ili kuondoa tatizo hilo, mimi nitachangia madawati
yaliyobakia kwa madarasa hayo matatu ili watoto wetu wakae vizuri,
wazingatie masomo yao na pia wawe na miandiko mizuri,” alisema huku
akishangiliwa na walimu, wanafunzi na baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo
waliohudhuria hafla hiyo.
Madawati hayo 135 na viti vyake vina thamani ya sh. milioni 11.5 kwa bei ya sh. 85,000/- kwa kila dawati na kiti chake.
Alipoulizwa ni lini madawati hayo yatakuwa tayari, Mtendaji
Mkuu wa kampuni hiyo, Bibi Rupa Suchak alisema yatawasilishwa shuleni
hapo baada ya wiki moja kwa sababu wana madawati ambayo
yamekwishatengenezwa kwenye bohari za kiwanda chao.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuongea na jumuiya
iliyofika kushuhudia utolewaji wa msaada huo, Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali, Bw. Ali Juma Shamhuna alisema yeye alisoma kwenye
shule hiyo mwaka 1952 na kuainisha kwamba wana uhaba wa madawati kwa
madarasa manne.
“Tunayo madarasa matupu manne na hii ndiyo skuli yangu
niliyosoma tangu mwaka 1952. Ni kweli tunakua na tunaongezeka lakini
bado tuna watoto wanakaa chini… wananchi wa Zanzibar wanajitolea kujenga
shule lakini inapofika kwenye madawati imekuwa ni tatizo. Tunaomba
kuungwa mkono zaidi”, alisema.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi, Bw. Ayoub Mahmoud
Jecha alisema shule hiyo ina shule za Serikali 64 lakini ni shule mbili
tu ndizo zina madarasa yaliyokamilika na yote yakiwa na madawati.
Alisema wilaya hiyo ina jumla ya wanafunzi 114,000 ambapo 79,000 kati
yao wanasoma kwenye shule za Serikali na 35,000 wanasoma kwenye shule za
binafsi.
“Wilaya hii ina upungufu wa madawati 5,700. Kwa uwiano wa
dawati moja kwa kila watoto watatu, ina maana kuwa watoto 17,100
wanasoma wakiwa wamekaa chini. Tunashukuru mchango huu wa Jambo Plastics
lakini tunaomba wahisani zaidi wa kutusadia ili watoto wetu wapate
mazingira mazuri ya kujifunzia,” aliongeza.
Awali, Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Jambo Plastics,
Bibi Rupa Suchak katika taarifa yake alisema kampuni yake imeamua
kutumia plastiki kutengeneza madawati kwa sababu imedhamiria kuhifadhi
mazingira lakini kuokoa kudorora kwa uchumi.
“Haya madawati ni imara na yanadumu kwa muda mrefu
tumeshayasambaza kwenye shule zaidi ya 400 huko Tanzania Bara na tumeona
matokeo mazuri… pia yanasaidia kuhifadhi mazingira kwa kuzuia ukataji
miti ovyo. Takwimu zinaonyesha miti zaidi ya 100,000 inakatwa kila mwaka
kwa ajili ya kupata mbao za kuetengezea madawati,” alisema.
“Madawati haya yanaweza kuongezwa au kupunguzwa urefu
kulingana kimo cha mtoto lakini pia yana uimara wa pekee ambao unaokoa
mamilioni ya fedha ambazo zingetumika kununua madawati mengine pindi
yale ya mbao yanapovunjika,” alisema.
Waziri Mkuu alirejea jijini Dar es Salaam jana jioni.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMAPILI, MEI 3, 2015.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...