Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba ameagiza taasisi zilizo chini ya wizara hiyo ziendeleze michezo kwa wafanyakazi wao makazini na kuhakikisha wanashiriki michuano  ya mashirika ya umma na taasisi zenye uwezo kama Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kushiriki Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.

Dk. Tizeba amesema hayo mwishoni mwa wiki Jijini Mwanza wakati akiwapongeza wanamichezo wa timu ya Wizara ya Uchukuzi iliyoshiriki michuano ya michezo ya Mei Mosi na kuibuka washindi wa jumla.

“Mnataka kuniambia Bakhressa (Salim Bakhressa, mmiliki wa timu soka ya Azam inayoshiriki Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara) ana fedha kuliko Bandari, “ Waziri Dk. Tizeba aliwauliza wanamichezo hao wakati akitia msisitizo kwa Mamlaka ya Bandari, shirika kubwa, kuwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu hiyo nchini.

Alisema timu za taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi na hasa zenye uwezo mkubwa wa kifedha kama Bandari zina fursa ya kushiriki hata Ligi Kuu kama ilivyo Azam ya Bakhressa. Alizitaka zijiandae mapema kwa michezo ya Mesi mosi kwa kuandaa michuano ya ndani na  ya taasisi ili kupata timu bora ya wizara. Alisema vikombe 12 ni vichache sana na akataka mwakani viwe zaidi ya 40 kwani uwezo huo wanao.

Aliwaeleza wanamichezo hao waliotwaa vikombe 12, vitano vya ushindi wa kwanza kuwa, michezo ni sehemu ya kazi na hivyo kumwagiza Mkurugenzi wa Raslimali Watu na Utawala(DAP) wa Wizara ya Uchukuzi, Immaculate Ngwalle kuwaagiza watendaji wa taasisi za wizara hiyo kuipa michezo umuhimu. 

Alisema ni aibu kwa taasisi nane tu kati ya 15 za Wizara hiyo kushiriki Mei mosi kwa madai ya ukata na kuwataka watendaji wa taasisi hizo kuhakikisha wanaweka bajeti ya michezo kwenye bajeti yao kuu vingnevo, hataipitisha kwani wafanyakazi wanapaswa kushiriki michezo kama sehemu ya kazi zao pia.

Aliwataka watendaji wa taasisi ambazo zimeajiri wafanyakazi wa muda kwa muda mrefu ambao ajira zao si za kudumu kuomba kibali cha ikama iii wathibitishwe kazini ili washiriki michezo hiyo bila utata kwani ni haki yao na huchangia ushindi kama walivyofanya kina mama wa Bandari walioshinda mchezo wa kuvuta kamba ingawa ni vibarua. Alihoji kama taasisi hizo haziwahitaji, vipi ziendelee nao muda mrefu.

Wanamichezo  100 wa timu ya Uchukuzi walioshiriki walitoka Bandari (TPA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga(TCAA), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Masuala ya Bahari (DMI) na Wizarani. TAA iliongoza kwa kutoa wanamichezo 56 ikifuatiwa na Bandari 26 na ya mwsho ni NIT (1).

Michezo waliyoshiriki ni soka walioyoibuka washindi wa tatu, baiskeli, netiboli, bao, kuvuta kamba, karata. Mbali ya Waziri, DAP, Mama Ngwalle aliwapongeza kwa ushindi huo mnono na kuwataka waongeze bidiii zaidi mwakani. Manahodha wa timu zilizoshinda walimkabidhi Dk. Tizeba vikombe vyao. IMETOLEWA NA GODFREY LUTEGO, AFISA UHUSIANO, MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...