Baadhi ya wananchi wakitafuta maeneo ya hifadhi
































Na Abou Shatry wa Swahili Villa

Familia zisizopungua 200 zimeachwa bila makaazi baada ya makaazi yao kuharibiwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyoikumba manispaa ya mji wa Unguja na vitongoji vyake.
Akizungumza na Swahilivilla kwa njia ya simu, mkaazi wa Mwanakwerekwe Sokoni, mjini Unguja ndugu Mussa Makame alisema kuwa mvua hizo zilizoendelea kwa muda wa siku mbili mfululizo, zimepelekea maafa makubwa katika miundombinu mjini humo.
"Hali ya hewa ya Zanzibar kwa siku ya pili leo imekuwa na utata wa hali ya mvua na maafa mengi yametokea", alisema Ndugu Mussa, na kuongeza kuwa kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa za watu wawili kupoteza maisha kutokana na maafa hayo, na kwamba vyombo rasmi vinavyohusika vitatoa taarifa sahihi kuhusu tetesi hizo katika wakati muafaka.
Aliendelea kusema kuwa wananchi wamekuwa wakishirikiana katika juhudi za kusaidia waathikika wa janga hili, na kwamba serikali imetenga makaazi ya muda katika mashule na kujenga mahema kwa ajili ya kuzihifadhi familia zilizoathirika vibaya. 
Aliyataja maeneo yaliyoathirika zaidi kuwa ni Mwanankwerekwe, Jang'ombe, Chumbuni na Tomondo. Aliutaja ujenzi holela na miundombinu duni kuwa ni miongoni mwa sababu zilizopelekea watu wengi kuathirika na mafuriko hayo.
Mbali na athari za kijamii, mvua hizo pia zimekuwa na athari za kiuchumi kwa vile barabara kuu inayounganisha mji wa Zanzibar na Mkoa wa Kusini Unguja zimekuwa hazipitiki. Hali hii imepelekea usumbufu kwa wafanyabiashara kutoka maeneo ya kisiwa cha Unguja kufika katika maeneo ya Mjini ambako ndiko kwenye harakati nyingi za kiuchumi.
Katika mahojiano hayo na Bwana Abou Shatry wa Swahilivilla, Ndugu Mussa amewataka Wazanzibari kuacha tofauti zao za kisiasa na kuwa kitu kimoja katika kukabiliana na maafa hayo. "Mvua ni kudura ya Mwenyezi Mungu, hakuna wa kulaumiwa, na wale wanaoingiza siasa waache kufanya hivyo", alisema Ndugu Mussa, na kuongeza kwamba tayari kuna watu wameanza kuingiza maslahi binafsi ya kisiasa katika swala hili.
Mafuriko haya yanakuja wakati Zanzibar ikiwa bado inaendelea kuuguza jeraha la kimbunga kilicholikumba eneo la Kisiwapanza, kisiwani Pemba wiki chache zilizopita.
Ungana nasi kusikiliza Mahojiano yetu na Ndugu Mussa Makame.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 05, 2015

    Hii hali siyo nzuri, wataalamu watafute ufumbuzi kuzuia mafuriko kama haya yenye hasara kwa wananchi na mali zao.

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 06, 2015

    Mafuriko hayazuiwi, ila unayapisha, usijenge kwenye njia ya maji!! Maji hayasahau njia yake hata ikipita miaka mia tano!! Hata kama umeendelea kiasi gani!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...