Na. Andrew Chimesela
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rajab Rutengwe amesema Pamoja na kuwa Mkoa wa
Morogoro una maeneo makubwa ya ardhi bado maeneo hayo hayajatumika ipasavyo na
kushiwishi wawekezaji kuja kuwekeza Mkoani humo katika Sekta ya kilimo, Viwanda na Utalii.
Dkt. Rutengwe ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa mazungumzo baina yake na Balozi
wa Afrika ya Kusini Nchini Tanzania Mhe T. D. Mseleku alipomtembelea Ofsini kwake.
Aidha, alimueleza Balozi Mseleku kuwa eneo ambalo halijatumika kikamilifu katika Sekta ya
kilimo ni kilimo cha umwagiliaji ambacho kwa Mkoa wa Morogoro kinawezekana kutokana na
Mkoa kuwa na mito mingi inayotitirisha maji kipindi chote cha mwaka.
Dkt. Rutengwe alisema, kwa jumla Mkoa wa Morogoro una maeneo makubwa, yenye rutuba na
yanayofaa kwa kilimo. Hata hivyo alibainisha kuwa ipo ardhi kubwa inayomilikiwa na Wananchi
ambao baadhi yao wameshindwa kuiendeleza na Serikali iko katika mchakato wa kuyachukua
maeneo hayo na kuyatoa kwa wawekezaji watakayoyaendeleza.
“Morogoro tuna ardhi kubwa na yenye rutuba lakini haijatumika inavyotakiwa, Serekali ipo
mbioni kubadilisha matumizi ya maeneo hayo ili kuwapa wawekezaji wanaoweza kuitumia ardhi
hiyo kikamilifu kwa faida ya wanaMorogoro na taifa” alisema Dkt. Rutengwe.
Kuhusu kushawishi wawekezaji wengi kuwekeza Mkoani Morogoro, alisema Mkoa unaandaa
kongamano la Uwekezaji ambalo linatarajiwa kufanyika hivi karibuni kongamano
litakalojumuisha Mikoa ya Morogoro na Pwani.
Kwa upande wake Balozi wa Afrika ya Kusini Hon. Mseleku alimshukuru Dkt. Rutengwe kwa
kuonesha ushirikiano na dhamira ya dhati ya kuwakaribisha wawekezaji na kuomba kuendeleza
ushirikiano wa pande hizo mbili uliokwishaanza.
Katika hatua nyingine Dkt. Rutengwe mara kadhaa amekuwa akishawishi watendaji katika
Mkoa wa Morogoro kuutangaza Mkoa kupitia vyombo vya Habari na mitandao mbalimbali ya
kijamii kam Blogs ili kuharakisha maendeleo ya Mkoa na watu wake kiuchumi na kijamii.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rajab Rutengwe (kulia) akimkaribisha Balozi wa Afika ya Kusini
Nchini, Bw. T.D. Mseleku alipomtembelea Ofsini kwake hivi karibuni.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rajab Rutengwe (kulia) akiwa katika mazungumzo na mgeni
wake Balozi wa Afrika Kusini Bw. T. Mseleku.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rajab Rutengwe (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Bw.
T. Mseleku Balozi wa Afirika ya Kusini mbele ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...