Benki ya Exim Tanzania imezindua kampeni maalum ya kuhamasisha wateja wake kufungua akaunti ya amana ya malengo (Fixed Deposit Account) ikiwa sehemu ya mpango wa benki hiyo kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba miongoni mwa watanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma lililopita, Meneja Bidhaa wa Benki hiyo, Bw Aloyse Maro alisema lengo kuu la kampeni hiyo ni kukuza utamaduni wa kuweka akiba hapa nchini ili kuongeza tija kwenye maendeleo ya taifa.
"Kampeni hii ina lengo la kukuza utamaduni wa kuweka akiba hapa nchini.Viwango vya ushindani vinavyotolewa na benki yetu ndio chachu ya mafanikio kwenye kampeni yetu hii kwakuwa kupitia akaunti hii wateja wetu wataweza kunufaika zaidi kwa kupata kiasi kikubwa cha faida mrejesho kutoka kwenye akaunti zao,’’ alibainisha Bw. Maro.
Katika jitihada za kuonyesha dhamira ya benki hiyo katika kuhamasisha zaidi ufunguaji wa akaunti hiyo, Bw. Maro aliongeza kuwa kampeni hiyo itaambatana na zawadi za kila mwezi kwa wateja watakaokuwa wanafungua akaunti hiyo.
"Zawadi hizi za kila mwezi ni pamoja na simu aina ya iphone. Pia tunatarajia kutoa zawadi ya gari kama tuzo kuu '' alitangaza meneja huyo kwa majigambo.
Bw. Maro alisisitiza zaidi kuwa Benki hiyo inadhamira ya dhati katika kuhakikisha kwamba wateja wake wanapata huduma na bidhaa bora zaidi za kibenki huku pia akitumia fursa hiyo kuwashawishi wateja wa benki hiyo kufika au kuwasiliana na matawi ya benki hiyo ili kupata maelezo zaidi kuhusu kampeni hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...