KAMISHENI ya Wachezaji wa Riadha, imepata viongozi wapya watakaoiongoza kwa miaka minne katika uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa shule ya Filbert Bayi, Mkuza Kibaha mkoani Pwani.
Kuundwa kwa Kamisheni za wachezaji kunatokana na agizo la Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC), ambako Bara la Afrika kupitia Anoca, iliagiza wanachama wake kutekeleza.
Lakini licha ya agizo hilo kutolewa, vyama na mashirikisho mengi yameshindwa kusimamia uanzishwaji wa Kamisheni hizo, ambazo ni kiungo muhimu kati ya wachezaji na Kamati za Utendaji za vyama na mashirikisho hayo.
Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Amani Ngoka wa Arusha ambaye alikuwa mgombea pekee, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti baada ya kupata kura 65 za ndiyo, 14 hapana huku sita zikiharibika.
Mchuano mkali ulikuwa kwenye nafasi ya Katibu, ambako Mwandu Jilala wa Dar es Salaam alishinda baada ya kupata kura 37 akifuatiwa na Adelina Trasius wa Dar es Salaam na Ezekiel Ngimba wa Arusha waliopata kura 18 kila mmoja huku Taratibu Machaku akiambulia kura tatu.
Wajumbe wawili wanaume walichaguliwa Emmanuel Giniki kutoka Manyara kura 67 na Gabriel Gerald wa Arusha wakati Elias Hotay pia wa Arusha kura hazikutosha baada ya kupata 38 huku kura mbili zikiharibika.
Kwa upande wa wanawake waliochaguliwa ni Pendo Pamba kura 67 na Highness Bampenja kura 65 wote kutoka Dar es Salaam.
Kabla ya uchaguzi huo Kamisheni hiyo ilikuwa chini ya uongozi wa John Yuda na Fabian Joseph.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...