EFM katika ubora wake wa kuhakikisha inawaletea burudani na
elimu watu wa rika zote, ina kipindi kiitwacho Zama Zile, kipindi hiki cha saa
tatu huwa hewani kila Jumapili kuanzia
saa mbili hadi saa tano usiku.
Kipindi hiki huendeshwa na mwanamuziki gwiji Anko John Kitime, ambaye ni mtunzi, mwimbaji, mpiga gitaa na pia ni mwanalibeneke aka blogger mahiri...
JOHN KITIME……Mwanamuziki
huyu ambaye alianza kupiga katika muziki katika bendi mwaka 1968, na ambae baba yake pia alikuwa mpiga gitaa aliyerekodi
mara ya kwanza TBC mwaka 1959, amesema kuwa katika kipindi chake yeye hupiga
muziki ambao aliusikia na hata kuucheza katika katika kipindi cha utoto wake na
ujana wake.
Katika kipindi hiki utaweza kusikia nyimbo ambazo si rahisi
kusikika katika zama hizi na pia kujua habari mbalimbali za nyimbo hizo.
Katika kipindi hiki cha Zama Zile pamoja na kusikia nyimbo
ambazo huchaguliwa na wasikilizaji, pia utasikia muziki uliokuwa ukipigwa kabla
ya kuingia vyombo vya muziki vilivyotumia umeme, muziki wa zamani kutoka mabara
yote duniani ambao uliweza kupenya na kupendwa katika anga za Tanzania, muziki
wa aina mbalimbali uliopigwa nchini bila
kusahau muziki wa taarab.
Ni hapa tu utaweza
kusikia sauti ya Siti Binti Sadi muimbaji wa kike wa kwanza kuwa ‘superstar’
Zanzibar, pia hapa utasikia nyimbo kutoka bendi maarufu kutoka mikoa mbalimbali
nchini, Mitonga Jazz ya Lindi, Kochoko Jazz ya Masasi, Mara Jazz, Super Veya ya
Mwanza, Lake Tanganyika Jazz na Kibisa za Kigoma, Mbeya Jazz, Zaire Success ya
Moshi na pia zikiwemo bendi zilizokuwa
za wanafunzi, kama Kwiro Secondary na Mkwawa high School. Hakika kipindi hiki
nisafari ya kihistoria kila wiki.
Je, unajua kuwa mtindo wa Fimbo Lugoda wa bendi ya Tancut
Almasi ulitokana na mwanamuziki mmoja kucharazwa mikwaju na mpenzi wake? Ulijua
kuwa mtindo wa Washawasha wa Maquis ulitokana na mcheza show wa Maquis
kudondokewa na washawasha? Unajua kuwa mtindo wa Bomoa Tutajenga kesho wa
Orchestra Mambo Bado ulitokana na geti kutaka kubomoka?
Usikose kusikiliza ZAMA ZILE kila Jumapili saa mbili mpaka
saa tano usiku EFM 93.7fm
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...