Na Makame Mshenga-
Maelezo Zanzibar
Wakulima wa zao la Karafuu wametakiwa kuacha tabia ya kuchukua Miche mingi ya Zao hilo ambayo wanashindwa kuishughulikia ipasavyo, kwani kwa kufanya hivyo ni kurudisha Juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuliimarisha zao hilo kwani Miche hiyo inagharimu kiasi kikubwa cha Pesa za kuitunza.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) Mwanahija Almas alipokuwa akizungumza na Wakulima wa Zao la Karafuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja katika Ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni.
Amesema inashangaza kuona baadhi ya Wakulima huchukua miche ambayo hawawezi kuihudumia vyema kwa vile tu hutolewa bure na Serikali, jambo ambalo hupelekea Miche hiyo Kufa.
“Tumesikia hapa katika Mijadala kuwa kuna baadhi ya Wakulima huchukua mpaka Miche 400 wakati hawana uwezo wa kuihudumia matokeo yake yote huangamia bila kuleta faida” Alisema Mkurugenzi Mwanahija.
Amewataka Wakulima hao kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali ili kuhakikisha ubora wa zao la Karafuu za Zanzibar unabakia ili kukidhi vigezo vya sifa vya Kimataifa.
Amesema lengo la Serikali katika kilimo cha zao la Karafuu ni kuona linaendelea kuwa tegemeo katika kuingiza fedha za kigeni na kusaidia kukuza Uchumi hivyo linahitaji kulindwa na kila Mwananchi kwa kuongeza uzalishaji na kulinda ubora wake.
Kwa upande wao Wakulima waliiomba Serikali kuendeleza ushirikiano na Wakulima hao ikiwa ni pamoja na kuongeza Bei ya zao hilo pale Soko la Kimataifa litakapoimarika.
Awali akitoa Mada Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wakulima wa Karafuu Zanzibar (ZACPO) Abuubakar Mohammed Ali alielezea umuhimu wa Jumuiya hiyo kuwa ni kuwa na Sauti ya Pamoja ya Wakulima katika kupigania Maslahi yao.
Sambamba na hilo Mohammed alisema malengo yao ni kuhakikisha kila Mkulima anamiliki Kitalu chake cha kuzalisha miche badala ya kuitegemea Miche inayotolewa na Serikali.
Akifunga Mkutano huo wa Wakulima wa Karafuu Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Juma Kassim Tindwa amesisitiza haja ya kuwepo Uadilifu baina ya Wakulima na Shirika la ZSTC ili kila upande unufaike.
Amewataka Wakulima hao kuhakikisha wanapeleka zao hilo katika Vituo halali vya Kuuzia ZSTC ili kuepuka aina yoyote ya Magendo.
Zao la Karafuu ni zao tegemezi katika uchumi wa Zanzibar ambalo pia huipatia Zanzibar Fedha za kigeni baada ya kuuzwa katika Soko la Dunia.
![]() |
Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja Mhe. Juma Kassim Tindwa akifungua Mkutano wa Wakulima wa zao la Karafuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja uliofanyika Chuo cha Amali Mkokotoni. |
Baadhi ya wakulima wa zao la karafuu wakifuatilia mkutano huo uliofanyika Chuo cha Amali Mkokotoni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya wakulima wa Karafuu (ZACPO) akifafanua kitu mara baada ya kulizwa swali na wakulima wa Karafuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja katika Mkutano wa wakulima wa zao hilo.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) Mwanahija Almas Ali akizungumza na wakulima wa zao la Karafuu katika Mkutano na wadau wa zao hilo huko Chuo cha Amali Mkokotoni.
Mkurugenzi Fedha (ZSTC) Ismail Omar Bai akitoa tathmini ya manunuzi ya Karafuu kwa upande wa Pemba kwa niaba ya Afisa Mzamini ZSTC Pemba katika Mkutano wa wazalishaji wa zao la karafu wa Mkoa Kaskazini Unguja. Picha na Makame Mshenga- Maelezo Zanzibar.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...