Halmashauri ya Mji Njombe imetoa msaada wa fedha wenye thamani ya
shilingi Million tano (5,000,000/=) kwa vikundi vya Wajasiriamali vya Watu
Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU), ambapo fedha hizo zitatumika
kuendeleza miradi mbalimbali iliyoanzishwa na iliyopendekezwa kuanzishwa
na vikundi hivyo.
Mratibu wa Ukimwi katika Halmashauri ya Mji Njombe Ndugu Daniel
Mwasongwe alisema, fedha hizo zimetolewa kwa lengo la kuviwezesha
vikundi hivyo kuongeza kipato ambacho kitawasaidia kuendesha maisha yao
ya kila siku, kuondokana na dhana ya utegemezi na kuimarisha umoja na
mshikamano miongoni mwa wanakikundi.
“Halmashauri ina vikundi vingi sana vya WAVIU ambavyo vinahitaji misaada
kama hii ili kuweza kukuza na kuendesha miradi yao. Lakini leo hii
tumeamua kutoa msaada huu wa fedha kwa baadhi ya vikundi kutokana na
ukweli usiofichika kuwa miradi yenu ipo wazi na inaonekana. Tumieni fedha
hizi kuendeleza miradi ambayo ni endelevu na ambayo mmeridhia kuianzisha
kama kikundi. Tutafika na kukagua ni hatua gani mmepiga baada ya kupokea
msaada huu.”Alisema mratibu huyo
Jumla ya Vikundi 6 vya WAVIU kutoka katika Kata tano ndani ya Halmashauri
ya Mji Njombe vimenufaika na Msaada huo. Vikundi hivyo ni pamoja na
Kikundi cha Matumaini kilichopo Kata ya Uwemba ambacho kilipewa fedha
Taslimu shilingi 800,000/= kwa ajili ya shughuli za ufugaji nyuki na kilimo
cha viazi, Kikundi cha Muungane kutoka Kata ya Uwemba ambacho kilipewa
fedha Taslimu shilingi 1,000,000/= kwa ajili ya shughuli za Ufugaji nyuki na
Kilimo cha viazi, Mwongozo kutoka kata ya Njombe Mjini ambacho kilipewa
shilingi 800,000/= kwa ajili ya Ufugaji Kuku wa Kienyeji, Tulindane kutoka
Kata ya Kifanya Shilingi 800,000/= kwa ajili ya Ufugaji Nyuki, Kikundi cha
Upendo kutoka Kata ya Mji Mwema Shilingi 600,000/= kwa ajili ya Upandaji
Miti na Kikundi cha Twitange kutoka Kata ya Matola Shilingi 1,000,000/=
kwa ajili ya Ufugaji wa Ngombe wa Maziwa.
Mratibu wa Ukimwi wa Halmashauri ya Mji Njombe ameiomba jamii, Asasi za
Kiserikali na Zisizo za Kiserikali kujitokeza kuvisaidia vikundi hivi vya WAVIU
kwa kuwapatia misaada mbalimbali popote pale Nchini na kuondokana na
dhana ya Kuwanyanyapaa na kutotambua mchango wao haswa katika
maswala ya Kiuchumi na Ujasiriamali.
Mratibu wa Ukimwi wa Halmashauri ya Mji Njombe Ndg. Daniel Mwasongwe (Kushoto) akihakiki kiasi cha fedha cha shilingi 600,000/= ambazo zilikabidhiwa kwa Kikundi cha Upendo. Kulia ni Mwenyekiti wa Kikundi hicho akijaza fomu ya kukiri kupokea msaada huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...