NA HAFIDH KIDO, Ukerewe

MWAKA 1995 kulikuwa na vuguvugu la vyama ya siasa kurithi kiti cha Rais wa awamu ya pili Ally Hassan Mwinyi, hasa ikizingatiwa ulikuwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi. Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichoshika dola pamoja na vyama vya upinzani kama NCCR-Mageuzi ya Augustino Lyatonga Mrema na Chama cha Wananchi (CUF), ni nani mwenye sifa ya kuongoza Tanzania.

Mambo yalikuwa mengi lakini udini na ukabila vilishika nafasi kubwa, Rais wa Kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere kwa kuwa wakati huo alikuwa mzee pekee aliyezungumza na Tanzania nzima pamoja na nchi jirani wakakaa kimya kumsikiliza, hivyo aliamua kuzungumza alipokutana na waandishi wa habari katika Hoteli ya Kilimanjaro.

Alisema mengi lakini lililobaki katika vichwa vya wengi nikiwemo mimi ni kuhusu sifa za rais aliyetakiwa wakati huo, Mwalimu alisema “Utakuta mtu anasema huyu sifa zooote anazo lakini mhh Mkara, ndio Mkara…” Jumatatu wiki hii nilibahatika kutembelea visiwa vya Ukerewe mkoani Mwanza, miongoni mwa visiwa nilivyotembelea ni Irugwa na Ukara halafu nikamalizia Ukerewe katika Kata ya Nansio nilipopitisha usiku.

Nilipofika Ukara mwangwi wa hotuba ya Mwalimu Nyerere ulinijia kuwa yeyote anaweza kuwa rais wa nchi, vigezo vya kuwa mtu wa hali ya chini au kutoka katika eneo duni na ukoo usiotajika haliangaliwi na wananchi.
Nimezunguka na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana katika mikoa tisa ya nchi hii, katika hiyo tisa nimezunguka wilaya na majimbo yote ya uchaguzi. Malalamiko makubwa waliyokuwa nayo wananchi ni maji, umeme na ardhi. Wabunge na Mawaziri hawafiki kwa wananchi kusikiliza matatizo yao.

Kila tulipopita malalamiko yaliyokuwepo huwezi kuamini kuwa eneo hilo lina kiongozi, serikali ina utaratibu wa namna mbili za kuongoza nchi kubwa namna hii; kwanza kuna mwakilishi nwa serikali kuu, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Mkoa na Wilaya (DAS na RAS).Halafu kuna mwakilishi wa serikali za mitaa, Mbunge, Diwani, Meya, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa na Mwenyekiti wa Kijiji.

Wote hao hawahangaiki kutatua matatizo ya wananchi wanasubiri mwaka wa uchaguzi ufike washughulikiane, mara nyingine wanapokutana katika vikao vya maamuzi kama baraza la madiwani na kikao cha Bunge, hakuna kinachofanyika zaidi ya kuonyeshana chama gani kina msemaji mzuri.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 02, 2015

    Nakubaliana na wewe kiongozi wa Tanzania anaweza kutoka seheme yoyote ya Tanzania. Nakubaliana na wewe pia kuwa wakuu wa wilaya mikoa na halmashauri mbalimbali wangekuwa wanafanya kazi kama inavyotakiwa hii nchi ingekuwa mbali sana. Tuombe neema ya Mungu tumalize uchaguzi kwa amani tupate kiongozi makini anayeitakia mema na maendeleo nchi hii awe na maono ya kuikwamua Tanzania kutokana na maendeleo duni hasa vijijini. Viongozi watakaochaguliwa katika ngazi zote wawe wabunge madiwani wakuu wa mikoa, wilaya na watendaji katika halmashauri wawe na malengo yanayopimika ya kuendeleza nchi na watu wake. Miaka mitano baadaye kulia lia kwa maisha duni, maji, umeme, vyoo, masoko, kuishie awamu hii. Viongozi wetu watayarishwe kuleta mabadiliko yanayoonekana.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 02, 2015

    Watanzania wengi wakiinuliwa kimapato, nchi itapata kodi zaidi kupitia bidhaa zitakazoweza kununuliwa. Kuongezeka kwa kodi kutatuwezesha kulipa madeni, na kuendeleza miradi mingi ikiwemo kupata pesa zaidi za kuongeza ajira kwa ajili ya mishahara , maisha ya mkazi yataboreshwa zaidi. Tunapoacha sehemu kubwa ya wananchi nje ya uchumi wa nchi pato haliwezi kuongezeka, bidhaa hazitanunuliwa, kodi hazitaongezeka, viongozi wapya waamke wawe na mikakati kuleta maendeleo kote nchini.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 02, 2015

    Mwezi uliyopita nilisikiliza kipindi cha BBC asubuhi mtanznia akiripoti kutoka Tanga katika ufukwe wa bahari kuna kaya ambazo kwa miaka mingi hazina choo wana jisitiri baharini, halafu mama mmoja akasema siku moja alienda kujisitiri akakimbizwa na mnyama. Niliposikia nilijiuliza viongozi wa kata wa sehemu hiyo na ngazi zingine wako wapi?, mitazamo ya viongozi wetu lazima ibadilike kuna maendeleo wanayoweza kuhamasisha ambayo hayahitaji fedha za kigeni ni kufanya tu wajibu wao na kuhamasisha wananchi kuboresha maisha yao.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...