Mwakilishi wa Benki ya Afrika (ADB) nchini Tanzania
Tonia Kandiero akizungumza na washiriki wa Warsha ya Kimataifa ya
Watakwimu kutoka nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya kiingereza juu
ya ushiriki wa ADB katika masuala ya Takwimu katika Bara la Afrika leo
jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. albina Chuwa
akiwakaribisha nchini Tanzania washiriki wa mkutano wa kimataifa wa
Watakwimu kutoka nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya kiingereza leo
jijini.Washiriki wa Warsha hiyo wanajadili na kubadilishana uzoefu
kuhusu Pato la Taifa.
Naibu Mkuu, Wizara ya Fedha Prof. Adolf Nkenda akifungua warsha ya siku
5 ya watakwimu kutoka nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya kiingereza
uliofanyika leo jijini Dar es salaam.
Washiriki wa Warsha hiyo ya kimataifa ya Watakwimu kutoka nchi za
Afrika zinazozungumza lugha ya kiingereza wakiwa katika picha ya pamoja
leo jijini Dar es salaam.
Na.Veronica Kazimoto- Dar es salaam.
SERIKALI
imesema kuwa itaendelea kuongeza uwazi katika matumizi ya takwimu
zinazokusanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini ili kukidhi vigezo na
malengo ya mfumo mpya uliowekwa na Umoja wa Mataifa wa mwaka 2008 wa
upataji wa takwimu za pato la Taifa.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa Warsha ya kimataifa ya siku 5 ya watakwimu kutoka
nchi za Afrika zinazozungumza Kiingereza, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya
Fedha Prof. Adolf Nkenda amesema kuwa Tanzania inaendelea kukusanya
takwimu mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya watunga Sera na wananchi.
Amesema
kwa kutambua na kuthamini mchango wa takwimu katika maendeleo, Serikali
imeamua kuingiza takwimu za ubora wa mazingira na takwimu za matumizi
ya simu za mkononi kwenye Pato la Taifa.
Amefafanua
kuwa, mabadiliko hayo yataiwezesha Tanzania kuwa na takwimu zenye
uhalisia kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanyika nchini na mchango wake
katika Pato la Taifa.
Prof.
Nkenda ametoa wito kwa washiriki wa warsha hiyo kuendelea kuzingatia
weledi katika utekeleaji wa majukumu yao ili waweze kutoa takwimu sahihi
zinazoonesha hali halisi ya tafiti zinazofanyika katika nchi zao.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt.
Albina Chuwa akizungumza na washiriki wa Mkutano huo wa Kimataifa
amesema kuwa Nchi za Afrika zinahitaji Takwimu sahihi ili ziweze
kuendelea.
Amesema Tanzania
imepiga hatua kwa kuweka kipaumbele katika shughuli mbalimbali za
Takwimu ikiwemo kusaini mkataba wa Takwimu wa Afrika kuhusu kuongeza
uwazi katika upatikanaji na matumizi ya takwimu zilizopo kwa Maendeleo
ya Taifa.
Ameeleza kuwa kupitia
Mfumo mpya wa Umoja wa Mataifa wa kutengeneza Pato la Taifa wa mwaka
2008, Tanzania imefanikiwa kuingiza shughuli mbalimbali katika Pato la
Taifa ambazo hapo awali hazikuwemo, zikihusisha shughuli za kitaalam za
Sayansi na Teknolojia pamoja na sanaa.
Ili
kufanikisha shughuli za takwimu Barani Afrika Dkt. Chuwa ameziomba
Serikali zote za Afrika kuutumia na kuheshimu Mkataba wa Afrika wa
Takwimu wa mwaka 2008 unaotoa kipaumbele katika uboreshaji wa shughuli
za Takwimu.
"Napenda kutumia fursa
hii kuziomba Serikali za Afrika kuzijengea uwezo Ofisi za Takwimu ili
ziwe na uwezo wa kuzalisha takwimu za masuala mbalimbali kwa muda mfupi
maana Takwimu ni sasa kwa ajili ya kukidhi mahitaji na matarajio ya
wananchi", amesisitiza Dkt. Chuwa.
Aidha,
ameongeza kuwa warsha hiyo ya siku 5 ambayo imewajumuisha watakwimu
kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
na baadhi ya nchi za Afrika Magharibi zikiwemo Ghana na Nigeria inalenga
kuwajengea uwezo washiriki hao kwa kuwa na uelewa wa pamoja katika
kukabiliana na changamoto mbalimbali za Takwimu katika nchi zao.
Naye
Mwakilishi wa Benki ya Afrika (ADB) nchini Tanzania Bi.Tonia Kandiero
amewataka washiriki wa warsha hiyo kuzingatia mfumo uliowekwa wa upataji
wa takwimu za Pato la Taifa ili kuwezesha uwepo wa takwimu sahihi za
maendeleo ya nchi husika.
Amesema
kuwa wingi wa washiriki wa warsha hiyo waliohudhuria kutoka nchi
mbalimbali za Afrika ni ishara tosha kuwa nchi zao zinathamini mchango
wa Takwimu katika kuleta maendeleo.
Amesema
Benki ya Afrika ambayo yeye ni mwakilishi wake itaendelea kushirikiana
na nchi za Afrika ili kuhakikisha kuwa Takwimu mbalimbali zikiwemo za
Watu na Makazi, Pato la Taifa na nyinginezo zinapatikana kwa wakati na
kuchangia maendeleo ya Afrika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...