Serikali imewataka madereva walioanza kupata mafunzo ya kuendesha mabasi yatakayotumika katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) kuzingatia mafunzo hayo ya kihistoria hapa nchini. 
Mafunzo hayo yaliyoanza jana ni moja ya matayarisho ya kuanza kwa mradi huo katika kipindi cha mpito mwezi Oktoba mwaka huu. 
Akifungua rasmi mafunzo hayo jana jijini Dar es Salaam, Waziri Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bi. Hawa Ghasia aliwataka madereva hao kuyapokea kwa bidii na umakini mkubwa. 
“Mafunzo haya yatawapa fursa ya kuweza kufanya kazi kwenye miradi mingine ya BRT kwani vigezo na mtaala wake ni wa kimataifa,” alisema wakati wa maadhimisho hayo katika eneo la Ubungo. 
Waziri Ghasia aliieleza kwamba mafunzo hayo ni ya kihistoria hapa nchini kwani kwa mara ya kwanza watapatikana madereva wenye leseni za kimataifa na kuwa mafunzo hayo yatahusu pia namna ya kuhudumia wateja. 
“Madereva hawa watajengewa weledi na nidhamu katika kazi yao ambayo kwa sasa inalalamikiwa sana na wananchi wakilalamikiwa kwa utovu wa nidhamu na kutotii sheria za barabarani,” alisema. 
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Meck Sadiki alisema kuzinduliwa kwa mafunzo hayo ni ushahidi wa dhamira ya serikali kutatua kero ya usafiri na msongamano wa magari jijini humo kupitia mradi wa BRT.
 “Mradi huu wa aina yake nchini na barani Afrika utatoa fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara kwa sekta binafsi ambayo ndio msingi wa maendeleo ya nchi,” alisema. 
Mafunzo hayo kwa madereva wazalendo yanafanyika baada ya kushinda usaili ulio endeshwa na wataalamu kutoka chuo cha ufundi stadi na mafunzo (VETA). Jumapili iliyopita kampuni ya watoa huduma wa ndani wa mradi huo, UDA-RT iliendesha semina ya mafunzo kwa wahariri wa vyombo vya habari kuhusiana na huduma za kipindi cha mpito za mradi huo. 
Mradi huo wa awamu ya kwanza unahusisha ujenzi wa kilometa 20.9 za barabara maalum kutoka Kimara hadi Kivukoni; barabara ya Msimbazi kutoka Faya hadi Kariakoo-Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa kuanzia Magomeni hadi eneo la makutano ya Morocco.
 Wakurugezi wa Kampuni ya UDA Rapid Transit, Bw. Robert Kisena (kulia) na Bw. Sabri Mabruk (kushoto) wakiwa katika moja ya basi la Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) pamoja na wahariri mbalimbali mara baada ya semina ya mafunzo kwa wahariri hao juu ya kuanza kwa kipindi cha mpito cha mradi huo mwezi wa Kumi mwaka huu.  Semina hiyo ilifanyika Jumapili jijini Dar es Salaam.
 Wakurugezi wa Kampuni ya UDA Rapid Transit, Bw. Robert Kisena (kulia) na Bw. Sabri Mabruk (kushoto) wakibadilishana mawazo nje ya moja ya basi la Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) mara baada ya semina ya mafunzo kwa wahariri hao juu ya kuanza kwa kipindi cha mpito cha mradi huo mwezi wa Kumi mwaka huu.  Semina hiyo ilifanyika Jumapili jijini Dar es Salaam.
 Mmoja wa Wakurugezi wa Kampuni ya UDA Rapid Transit, Bw. Sabri Mabruk (wa nne kushoto) akiwalekeza jambo wahariri mbalimbali wakati wa semina ya mafunzo kwa wahariri hao kuhusu kuanza kwa kipindi cha mpito cha mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT).  Semina hiyo ilifanyika Jumapili jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Haya ni maendeleo makubwa katika jiji letu la Dar-es-Salaam ambayo lazima yapongezwe yanapofikia hatu hii, na zijazo za kurahisisha usafiri na kuufanya wa kiungwana zaidi. Utumiaji wa kadi utatuvusha kwenye ligi ya majiji ya kidijitali.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...