WAZIRI wa
Nishati na Madini, George Simbachawene ameiasa Kamati ya Pamoja ya
Uendeshaji wa Mgodi wa TanzaniteOne, “Joint
Operating Committee”-JOC
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ili kuwanufaisha wadau wa Tanzanite katika uvunaji wa madini hayo, huku
wakilinda maslahi ya mgodi huo kwa Taifa.
Simbachawene ametoa rai hiyo hivi karibuni wakati akizindua Kamati ya hiyo ya JOC, katika hafla iliyofanyika kwenye eneo
la mgodi wa TanzaniteOne uliopo Mirerani, katika Wilaya ya Simanjiro mkoani
Manyara.
“Suala la kulinda
maslahi mapana ya mgodi huu kwa Wabia na Taifa linawezekana, iwapo Wanakamati
ya JOC mtafanya kazi kama timu kwa
kila mmoja kutimiza wajibu wake ipasavyo. Hivyo basi ipokeeni kazi hii na
kuitekeleza kwa ari, kasi na nguvu kubwa” Alisisitiza Mh. Simbachawene.
Ameigiza Kamati hiyo ya JOC kukamilisha
majadiliano ya kuboresha Mkataba wa ubia uliokuwepo baina ya STAMICO na TML
kwani mabadiliko ya Mkataba huo yataleta matokeo chanya katika udhibiti na
uendelezaji wa mgodi na biashara nzima ya Tanzanite kwa manufaa ya wabia wote
na Taifa pia.
“Baadhi
ya vipengele vinavyohitaji kuboreshwa ni pamoja na suala la kutangaza
chimbuko la Tanzanite duniani kuwa ni Tanzania; kuimarisha mazingira ya mgodi
kuwa kivutio cha utalii na mafunzo; kuchangia huduma za jamii zinazozunguka
mgodi na kupanda miti katika maeneo ya mgodi ili kutunza mazingira” alifafanua
Mh. Simbachawene.
Kamati
hiyo ya JOC ina wajumbe 6 ambao ni Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO; Bi. Asha Jumanne
Ngoma, Prof. Peter Antony Kopoka kwa upande wa STAMICO na Bwana Faisal Juma
Shahbhai, Bwana Hussein Omary Gong’a na
Bwana Halfan Mpenziye Hayeshi kwa upande wa Sky Associates Ltd. Kamati hii
inaongozwa na Bwana Faisal Juma Shahbhai.
Katika uzinduzi wa Kamati hiyo, Mheshimiwa
Simbachawene pia aliwakumbusha wajumbe wa Kamati ya JOC kumsimamia kikamilifu
mwendeshaji wa mgodi huo yaani TML ili aweze kutekeleza masharti ya mkataba wa
ubia katika uzalishaji wa Tanzanite, kwa manufaa ya pande zote.
Aidha amewasisitiza wajumbe wa JOC kufanya
maamuzi yenye tija katika uidhinishaji wa bajeti, kubuni mipango ya maendeleo
ya mgodi; kuandaa sera za uendeshaji; kuunda kamati za ushauri kulingana na
mahitaji na kuingia makubaliano ya pamoja na Kitengo cha Uangalizi na Usimamizi
(Monitoring and Evaluation Unit), kuhusu mfumo wa uendeshaji mgodi, ili
kuongeza uzalishaji wa tanzanite na
kukuza soko la ndani.
Ameitaka Sky
Associates kutoa nafasi za ajira kwa Watanzania bila ubaguzi na kuzingatia
misingi ya utawala bora katika uendeshaji
wa mgodi huo huku wakitoa maslahi bora kwa wafanyakazi wake.
Simbachawene
amesema STAMICO kwa upande wake, haina budi kuwapatia Wafanyakazi wake waliopo
Mirerani vitendea kazi stahili ili wasiwe na kisingizio cha kushindwa
kutekeleza majukumu yao, na ameitaka Menejimenti ya Shirika hilo ipime utendaji
kazi wa wafanyakazi wake mara kwa mara ili kukuza ufanisi.
Kuhusu suala la
kuboresha mahusiano mazuri na Wachimbaji wadogo, Simbachawene amesema mahusiano
kati ya TanzaniteOne na Wachimbaji Wadogo yaendelee kuimarishwa, na amekiri
kuitambua Kamati Maalum iliyoundwa na Kamishna wa Madini, ili kuisaidia
Serikali kuweka mfumo mzuri wa uchimbaji katika mgodi huo, jambo ambalo
litaepusha ajali na kupunguza migogoro baina ya wadau.
“Nazitambua
changamoto za wizi na utoroshaji wa madini ya Tanzanite ambazo ni matokeo ya
wadau wasio waaminifu; nichukue fursa hii kuwataarifu kuwa Serikali imefanya
marekebisho ya Kifungu cha 6(4) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Kifungu
hicho sasa kinampa Kamishna wa Madini mamlaka kamili ya kutaifisha na kupiga
mnada madini yanayokamatwa yakimilikiwa kinyume cha Sheria. Hivyo, wote wenye
tabia ya kufanya biashara ya madini kinyume cha Sheria wajiandae kupoteza
madini yao” Aliongeza kwa msisitizo Mh. Simbachawene.
Awali,
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Bwana Deusdedith Magala amemshukuru Mh.
Simbachawene kwa kuunda Kamati hiyo ya JOC na kuizindua rasmi, kwani itasaidia kulinda hisa za STAMICO, za Serikali na mali
za mgodi, na pia kuuwezesha mgodi kufanya maamuzi makubwa na yenye tija.
Bwana
Magala amesema tangu Juni 2013 STAMICO ilipoingia
ubia wa umiliki wa mgodi wa TanzaniteOne na kampuni ya TML kwa uwiano wa
50:50 wa leseni ya uchimbaji wa Tanzanite, Bodi za Wakurugenzi za wabia
hao wawili ndio zimekuwa zikifanya kazi kama Kamati ya JOC, jambo ambalo
lilileta mzigo mkubwa wa kazi kwa bodi hizo.
Katika hafla hiyo
ya uzinduzi wa Kamati ya Ushirikiano ya Mgodi wa TanzaniteOne, Mh. Simbachawene
na ujumbe wake pia walikagua shughuli za uchimbaji wa Tanzanite katika mgodi wa
CT, zikiwemo uchorongaji, uchotaji na utoaji wa udongo na kujionea athari za
kimazingira zilizosababishwa na wachimbaji wadogo kwenye kitalu C.
Hafla hiyo ya uzinduzi wa JOC ilihudhuriwa na
mwakilishi wa Kamishna wa Madini Tanzania, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa
STAMICO, Wakurugenzi wa Kampuni ya Sky Associates Ltd na TML, Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Kamishna Msaidizi wa
Madini - Kanda ya Kaskazini, Wajumbe wa Kamati ya Pamoja ya Uendeshaji (JOC) na
Waandishi wa Habari.
Waziri wa Nishati na Madini,
George Simbachawene (aliyevaa miwani) akipata maelezo kuhusu uchimbaji, ndani
ya shimo la mgodi wa chini (underground
mine) wa TanzaniteOne wakati alipotembelea mgodi, kabla ya kuzindua Kamati
ya Pamoja ya Uendeshaji mgodi huo (JOC).
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene
(aliyekaa katikati) katika picha na Wajumbe wa Kamati ya Pamoja ya Uendeshaji “Joint Operating Committee – (JOC) ” ya
mgodi wa TanzaniteOne, baada ya kuizundua Kamati hiyo mgodini hapo mwishoni mwa
wiki. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa JOC Bwana
Faisal Juma Shahbhai na kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Duesdedith Magala. Wajumbe wengine waliokaa kutoka kushoto ni Asha
Jumanne Ngoma, Prof. Peter Antony Kopoka (wa tano), Bwana Hussein Omary Gong’a
(aliyesimama kushoto) na Bwana Halfan Mpenziye Hayeshi (aliyesimama kulia).
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene
(mwenye overall ya Kibluu) akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya JOC, Faisal Juma Shahbhai (aliyevaa
kofia ngumu ya Kibluu) kuhusu uzalishaji
wa Tanzanite katika mgodi wa TanzaniteOne. Anayemsikiliza (mwenye overall
ya Kijani) ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Duesdedith Magala.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...