BENKI ya Exim Tanzania imesaini
makubalino ya mkopo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 20 (takribani
42bn/-) na kampuni binafsi ya ukopeshaji ya nchini Ujerumani, Deutsche
Investitions und Entwicklungsgesellschaft
MBH (DEG), lengo likiwa ni kusaidia kuinua sekta ya biashara ndogo hapa
nchini(SMEs).
Kwa mujibu wa Afisa Mkuu wa Fedha wa
Benki ya hiyo, Bw. Selemani Ponda fedha
hizo zilizo katika mfumo wa mkopo mkubwa,
zitatolewa kwa awamu mbili kwa kuzingatia maendeleo ya ukuaji katika kusaidia sekta hiyo.
“Mkopo huu mkubwa unakuja wakati
muafaka ambapo uchumi unazidi kuimarika huku tukishuhudia mapinduzi makubwa ya
kibiashara. Biashara ndogo zinafanya jitihada za kila namna viingie katika
kundi la kati.
Huu ni wakati sahihi kwa benki yetu kuongeza nguvu katika sekta
hii,” alisema Bw. Ponda katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari jijini
Dar es Salaam mwishoni mwa juma lilipita.
Alisema kuwa benki hiyo imeendelea
kuwekeza katika kufanya tafiti na kuelewa mahitaji ya wafanyabiashara wadogo
hapa nchini jambo lililoiwezesha benki hiyo kubuni bidhaa na huduma zinazokidhi
mahitaji ya viwanda hivyo.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za benki hiyo
hadi kufikia sasa imekopesha jumla ya Tsh. 582bn/- huku 291bn/- kati ya kiasi
hicho zikiwa zimetolewa kwa sekta ya biashara ndogo na zile za kati.
Bw. Ponda alisema kuwa benki hiyo
inaona fursa ya kipekee kutoa mikopo katika sekta hiyo muhimu wakati ambapo kuna maendeleo makubwa ya
kiuchumi nchini.
Alibainisha kuwa benki hiyo, kwa zaidi
ya muongo mmoja, imeendelea kuimarisha uhusiano mzuri na taasisi za kimataifa
za kufadhili maendeleo ikiwa ni pamoja na IFC, PROPARCO, NORFUND na FMO.
“Kwa kusaini makubaliano haya na DEG,
inadhihirisha jinsi ambavyo taasisi hizi za kimataifa za kufadhili maendeleo
zina imani na benki yetu,” alisema kwa kujiamini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa taasisi
za fedha barani Afrika na Amerika Kusini kutoka kampuni hiyo ya DEG Bi. Gudrun
Busch alisema mkopo huo utasaidia kuongeza nguvu katika kuleta maendeleo kwenye
sekta ya biashara ndogo na za kati kote nchini na utasaidia kutatua changamoto mbalimbali
katika ukuaji wa uchumi,
“Kwa kufanya hivi, tutakuwa tumechangia
katika kuimarisha sekta ya uchumi nchini Tanzania na kutengeneza na kulinda
ajira,’’ aliongeza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...