Na Mwandishi Maalum, New York 
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amewaasa Maspika wa Mabunge Duniani kuhakikisha kwamba wanakuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa Malengo na Ajenda Mpya za Maendeleo Endelevu, kwa kushirikiana na Serikali zao na Asasi za Kijamii. 
“ Mnakutana katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ya wimbi kubwa la wakimbizi wanaokimbia vita na machafuko katika nchi zao, wimbi ambalo halijawahi kutokea tangu vita kuu ya pili ya dunia”. 
Ban Ki Moon ameyasema hayo siku ya jumatatu wakati akifungua mkutano wa Nne wa Maspika wa Mabunge Duniani ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano. Mkutano huu wa siku tatu unafanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na umeandaliwa na Chama cha Kimataifa cha Wabunge ( IPU). Na kuongeza. 
“ Tunachagizwa kuimarisha jitihada na juhudi za kuhubiri Amani, usalama, maendeleo endelevu na haki za binadamu duniani kote. 
“ Watu wanataka elimu, wanataka huduma bora za afya, na fursa zaidi za ajira. Wanataka kuishi pasipo kuwa na hofu. Wanataka kuziamini Serikali zao na Taasisi zake. Wanataka kuheshimiwa kwa haki za binadamu na haki ya kuzungumza na kusikilizwa katika maamuzi yanayohusu maisha yao” akasema Ban ki Moon. 
 Maspika wanaohudhuria mkutano huu, wanatoka katika mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea. Ujumbe wa Tanzania, unaongozwa na Mhe. Ann Mapinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
“Na pengine jambo muhimu kwenu na ambalo linawiana na majukumu yenu ni hili. Hiki ni kipindi ambacho mifumo ya kiserikali katika sehemu kubwa ya dunia inakabiliwa na changamoto ya kukosa kuaminiwa, uwakilishi na ushiriki” anaeleza katibu Mkuu 
Akizungumzia kuhusu ajenda na malengo mapya ya maendeleo, Ban Ki Moon amesema kuwa malengo hayo ambayo yapo 17 yamelenga zaidi katika maisha ya watu na sayari dunia. Na yanatoa mpango wa utekelezaji katika kumaliza umaskini, njaa na kujenga maisha yenye hadhi kwa wote bila ya kumwacha yeyote nyuma. 
 Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema lengo namba 16 linazungumzia demokrasia, kwa kutoa wito jamii na taasisi jumuishi. Na kwamba suala la demkorasia limetawala katika andiko lote la malengo mapya ya maendeleo kama upinde wa fedha kwa kutia msisitizo wa upatikanaji wa raslimali, huduma za afya, elimu na fursa za ajira na zenye hadhi kwa wote. 
Akasisitiza kwamba kazi ya kutekeleza na kusimamia malengo haya ni kubwa, inayohitaji Serikali kufanya kazi na kwa ushirikiano wa karibu na Asasi za Kijamii, uhusiano ambao anasema ama unatoweka ama haupo kutokana na baadhi ya nchi kuweka masharti magumu dhidi Asasi za Kijamii.
 Mbali ya Ban Ki Moon, viongozi wengine waliozungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huu wa Maspika wa Mabunge ni pamoja na Rais wa Baraza Kuu la 69 la Umoja wa Mataifa. 
 Baada ya ufunguzi Maspika waliendelea na majadiliano ya jumla yaliyojikita katika maudhui ya Amani, demokrasia na maendeleo endelevu.
  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon,  akifungua mkutano wa Nne wa  Maspika wa Mabunge  Duniani, siku ya Jumatatu, kulia kwake ni Rais wa IPU   Bw.  Saber Chowdhury na Katibu Mkuu wa IPU Bw. Martin Chungong  
 Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Ann Makinda akiwa na ujumbe wake  akifuatilia kwa makini hotuba za  ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Maspika wa  Mabunge Duniani ulioanza siku ya jumatatu hapa Makao  Makuu ya Umoja wa mataifa
Maspika wa Mabunge kutoka  Mataifa yanayoendelea na  yaliyoendelea wakiwa katika  ufunguzi wa Mkutano wao wa Nne ambao  hufanyika kila baada ya miaka  mitano. Ufunguzi wa Mkutano huu umefanyika katika Ukumbi Mkuu wa  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...