Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akizungumza wakati akizindua Malengo Endelevu 17 ya Maendeleo nchini (SDG’s) Tanzania katika shule ya Uhuru mchanganyiko, katika hafla ambayo pia benki ya Standard Chartered Tanzania ilishiriki na kugawa vitu mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo. (Picha na Zainul Mzige wa Modewjiblog)
Na Mwandishi wetu
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, amesema uondoaji umaskini nchini unawezekana kwa ushirikiano kati ya wadau mbalimbali wa maendeleo.
Kauli hiyo ameitoa mwishoni mwa wiki wakati akizindua Malengo Endelevu 17 ya Maendeleo nchini (SDG’s) Tanzania katika shule ya Uhuru mchanganyiko, katika hafla ambayo pia benki ya Standard Chartered ilishiriki na kugawa vitu mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo.
Katika hafla hiyo ambayo ilitengenezwa mahususi kuanzisha utekelezaji wa Malengo Endelevu (SDG’s) yakiwemo ya elimu, afya na mazingira Standard walipeleka miti 150 ya kupanda, kompyuta na pia kutumia muda kuangalia afya za wanafunzi.
Alisema katika kukabiliana na umaskini kwa kuangalia Maendeleo Endelevu hakuna kitu kigumu ukilinganisha na ugumu wa mwanafunzi asiyeona kujifunza kwa kupitia vitabu vya nukta nundu na asiyesikia kuwasiliana na mtu mwingine lakini pamoja na ugumu huo watoto hao wanaweza.
Alisema kwa ushirikiano wa wadau kama walivyofanya wao na benki ya Standard Chartered Tanzania anaamini kwamba maendeleo yatafikiwa na Tanzania itafanikiwa kuzika umaskini ifikapo mwaka 2030.
Alisema kutiwa saini kwa Malengo Endelevu na viongozi wa nchi 190 kumeonesha wazi nia ya seriakli mbalimbali duniani kushughulikia umaskini na kuuzika kwa kutekeleza malengo hayo endelevu.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Benki ya Standard Chartered Tanzania, Charles Katongole akitoa salamu za Mkurugenzi wake ambapo benki hiyo imeahidi kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha utekelezaji wa malengo mapya ya Maendeleo Endelevu (SDG's) yanafanikiwa nchini Tanzania. Kushoto ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania Hoyce Temu (kulia) pamoja na Mkuu wa Mahusiano wa benki ya Standard Chartered Tanzania, Juanita Mramba (wa pili kulia).
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Benki ya Standard Chartered Tanzania, Charles Katongole, alisema kwamba ni lengo la benki hiyo ni kurejesha faida kwa jamii kupitia miradi yake mbalimbali na kwamba kusaidia shule hiyo ya Uhuru mchanganyiko iliyoanzishwa 01-01-1921 awali ikiitwa Government African secondary school kabla ya kuhamishiwa Mzumbe Morogoro 01-01-1953 na kubadilishwa jina kuwa Kichwele African boys middle school ikiwa na madarasa ya V-VII, ni sehemu ya kurejesha faida kwa jamii.
Alisema ni lengo la benki hiyo kwa mwaka huu kuwezesha kupatikana kwa dola za Marekani milioni 5 kusaidia mambo mbalimbali ya watoto kwa mwaka huu kwa nchi za Afrika mashariki huku Tanzania pekee watoto milioni 10 wakifikiwa.
Benki hiyo yenye matawi Dar es salaam, Mwanza na Arusha katika miradi yake ya afya, vijana na elimu wamekusudia kushirikiana na Umoja wa Mataifa kutekeleza malengo mbalimbali endelevu ikiamini kwamba jamii ikiboreshwa itakuwa katika mfumo mzuri wa maendeleo na kupiga vita umaskini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...