Na Mwandishi Maalum, New York
Rais Jakaya Mrisho
Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa Jopo la
Ngazi ya Juu kuhusu Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya, anatarajiwa Ijumaa wiki
hii, kueleza mbele ya wajumbe wa nchi
wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo ya kazi ya jopo
hilo tangu kuundwa kwake.
Jopo la Ngazi ya juu kuhusu
mwitiko wa Kimataifa wa majanga ya kiafya
liliundwa mwezi wa nne mwaka huu
na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban
Ki Moon, ambapo Rais Kikwete
amepewa jukumu la kuongoza jopo hilo.
Taarifa ambazo zimeufikia Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, zimebainisha kuwa Mhe. Rais atawazungumza wajumbe wa
nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mara
baada ya kumalizika kwa mkutano wa tatu wa jopo hilo
unaofanyika hapa Makao Makuu ya
Umoja wa Mataifa.
Wajumbe wengine wa Jopo hili ni Bw. Celso Amorim ( Brazil), Micheline Calmy (
Switzerland), Marty Natalegawa (
Indonesia) Joy Phumapi ( Botswana) na
Rajav Shah ( USA).
Jukumu kubwa ya
jopo hilo kwa mujibu wa hadidu za
rejea, pamoja na mambo mengine, ni kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa katika kuzuia na kukabiliana na majanga ya kiafya ikiwa ni pamoja na kujifunza
kuhusu mwitikio wa Jumuiya ya Kimataifa
kufuatia kuibuka kwa janga
la ugonjwa wa Ebola.
Katika utekelezaji wa majukumu
yake Jopo limekuwa likikutana na kufanya
majadiliano ya kina na makundi mbalimbali yakiwamo ya wataalamu, wawakilishi wa
nchi tatu ambazo zimeathirika
sana na ugonjwa wa ebola ( Liberia, Siera Leone na Guinea),Mashirika ya Kimataifa
na Kikanda , Taasisi za Fedha za kimataifa, wahudumu wa Afya, Wasomi ,
Watafiti, Sekta Binafsi na wataalam wa fani na
kada mbalimbali.
Pamoja na kuhudhuria na kuongoza
mikutano ya Jopo, Mhe, Rais
Kikwete akiwa hapa Makao
Makuu ya Umoja wa Mataifa, pia atahudhuria Mikutano Mikubwa miwili ambayo
ni, Mkutano wa Kilele wa Kisiasa,
ambao Wakuu wa Nchi na Serikali watapisha
Malengo ya Maendeleo Endelevu ( SDGs). Mhe. Rais
atazungumza katika mkutano huu muhimu kwa mstakabali wa maendeleo na ustawi wa
binadamu kwa miaka 15 ijayo.
Malengo Mapya ya Maendeleo
yanachukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo
ya Millenia ( MDGs) yanayomaliza muda wake mwishoni mwa mwaka.
Aidha Mhe. Rais atashiriki na kuhudhuria Mkutano
wa 70 wa
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Na anaratajiwa kulizungumza
Baraza Kuu na hii itakuwa ni hotuba yake ya mwisho akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vile vile Mhe. Rais atahudhuria
mikutano mingine kadhaa.
Baadhi ya mikutano hiyo ni
ule ambao umeandaliwa kwa
pamoja baina ya Kansela wa Ujerumani Mhe. Angela Merkel , Waziri Mkuu wa Norway
Mhe. Erna Solberg na Rais wa Ghana Mhe.
John Dramani Mahama.
Mhe Rais anahudhuria
mkutano huu kwa mwaliko rasmi aliopewa
na Kansela Angela Markel. Washirika na
waandaji wengine wa mkutano huu ni Mfuko wa Bill na Melinda Gates, Shirika
la Afya Dunia ( WHO) na Bank ya Dunia.
Mkutano huu unatarajiwa kuzindua
misingi na hatua muhimu ambazo kwayo zitaratibu
ufanisi na upimaji
wa matokeo ya juhudi za kuimarisha mifumo ya afya.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...