DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
·
Aunga
mkono asilimia 100 staili ya Kampeni ya Magufuli
·
Asema
Tanzania inahitaji mawazo mapya ili iweze kusonga mbele
·
Atamani
muda wake wa kuongoza Tanzania kumalizika haraka zaidi
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa kama wapo watu
binafsi ama taasisi yoyote mahali popote wenye matatizo na Sheria ya Takwimu
mpya ama Muswada wa Habari nchini basi wawasilishe mapendekezo yake Serikalini
ili yafanyiwe kazi badala ya kukaa na kulalamika pembeni ama kwenye vyombo vya
habari.
Rais
Kikwete pia amesema kuwa ni jambo zuri na jema kuwa Mgombea Urais wa Tanzania
kwa tiketi ya CCM anaelezea fikra na matumaini ya kuleta mabadiliko makubwa zaidi katika uendeshaji wa
Tanzania tofauti na uendeshaji huo ulivyo chini ya uongozi wake.
Vile
vile, Rais Kikwete amesema kuwa anatamani muda uende kwa kasi zaidi ili aweze
kukabidhi madaraka ya kuongoza Tanzania kwa Rais wa Tano, ili yeye apate muda wa kumpumzika baada ya
kazi ngumu ya miaka 10 ambayo ameilezea kama mzigo mkubwa.
Rais
Kikwete ameyasema hayo, Jumanne, Septemba 22, 2015 wakati alipozungumza na
wafanyakazi wa taasisi nne za Marekani
ambazo kwa namna moja ama nyingine zimefanya kazi na Serikali yake katika
miaka 10 ya uongozi wake mjini Washington, D.C., ambako Rais amefanya ziara ya
siku mbili ya kikazi.
Rais
Kikwete amezungumza na wafanyakazi wa taasisi za National Democratic Institute
(NDI) yenye uhusiano na chama cha siasa cha Democratic, International
Republican Institute (IRI) yenye uhusiano na chama cha siasa cha Republican,
International
Foundation for Electoral Systems (IFES) na United States Institute of Peace
(USIP) kwenye makao makuu ya NDI.
Wakati
wa kipindi cha maswali na majibu na wafanyakazi wa taasisi hizo, Rais Kikwete
ameulizwa swali kuhusu madai kuwa Sheria ya Takwimu na Muswada wa Habari
inavuruga sifa za kidemokrasia za Tanzania chini ya uongozi wa Rais Kikwete.
Akijibu
swali hilo, Rais Kikwete amesema: “Nimelizungumza hilo huko nyuma na napenda
kurudia. Sheria ya Takwimu inahusu tu takwimu rasmi za Serikali na wala si
takwimu zote. Pili Sheria hii inatokana na matakwa na taratibu za Umoja wa
Mataifa na Sheria yetu imetungwa kwa kutilia maanani matakwa ya kimataifa ya
Umoja wa Mataifa. Kwa nini hili linakuwa tatizo kwa Tanzania pekee ni jambo
gumu kueleza.”
Kuhusu
Muswada wa Sheria ya Habari, Rais Kikwete amesema: “Nimelisema hili huko nyuma
lakini inaelekea halijaeleweka. Nilipata kusema pale Dar es Salaam na hata
wakati nazungumza na wabunge wa Sweden mjini Stockholm kuwa kama mtu ana tatizo
ama maoni na maudhui ya Muswada ule basi ayafikishe Serikali. Tutafanyia kazi.
Hakuna tatizo na jambo hili. Ajabu ni kwamba tunachosikia ni malalamiko tu na
hakuna yoyote ambaye amefikisha maoni yake kwetu.”
Hata
hivyo, Rais Kikwete ameongeza: “Jambo muhimu ambalo lazima sote tuelewane hapa
ni kwamba Muswada wowote, uwe wa habari ama wa jambo jingine, ni lazima ulinde
maslahi ya nchi yetu, yalinde umoja wetu, yalinde utulivu wa nchi yetu na yalinde
usalama wa nchi yetu. Haya ni mambo ambayo hatuna haja ya kujadiliana na yoyote
kwa sababu nchi zote duniani zinalinda kwa namna hii na zinaendeshwa namna
hii.”
Rais
Kikwete pia ameunga mkono mwenendo wa mgombea urais wa CCM wakati wa kampeni ya
Uchaguzi mkuu inayoendelea nchini, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli,
akisema: “Wamepata kuja watu kwangu… wakaniambia kuwa Mgombea wetu wa CCM
anashutumu na kusahihisha Serikali yangu na utendaji wake kwenye mikutano ya
kampeni. Niliwaambia hivi…..analofanya
Mgombea wetu ni jambo sahihi na barabara kabisa na lazima afanye hivyo.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Niliwaambia nchi yetu inahitaji mawazo mapya na mwelekeo mpya ulio tofauti
na uongozi wangu. Niliwambia kuwa tuliporuhusu jambo hilo kufanyika, nchi yetu
itabakia pale pale ambako nimeifikisha mimi. Haya yatakuwa na makosa makubwa
kwa sababu nchi yetu lazima isonge mbele kwa mawazo mapya, kwa uongozi mpya na kwa
staili mpya ya uongozi. Na haya ndiyo anayasema Mgombea wetu.
Vinginevyo ni
jambo lisilokuwa na maana kubadilisha uongozi kama hatuko tayari kukubali kuwa
kila kiongozi lazima awe na staili yake ya uongozi na namna yake ya kuongoza na
kuendesha nchi yetu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
24
Septemba, 2015
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...