Mikataba ya madini, gesi, mafuta kupitiwa na timu ya wataalam kabla ya kusainiwa. Na Greyson Mwase, Morogoro Ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Tanzania wananufaika na rasilimali za madini mbalimbali pamoja na gesi iliyogunduliwa kwa wingi hivi karibuni, Serikali imeanza kutoa mafunzo kwa wataalam kutoka taasisi za serikali watakaohusika na upitiaji wa mikataba yote ya shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini, gesi na mafuta kabla ya kusainiwa. 
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene katika uzinduzi wa warsha kuhusu dira mpya ya madini Afrika iliyofanyika mjini Morogoro. 
Warsha hiyo ya siku tatu iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini ilikutanisha wataalam kutoka taasisi za serikali ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais- Tume ya Mipango, Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) 
Pia ilikutanisha wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na taasisi zake kama vile Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Shirika la Uendelezaji Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mpango wa Kuongeza Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji Nchini (TEITI), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Chuo cha Madini Dodoma (MRI). 
Simbachawene alisema uundaji wa timu ya wataalam mbalimbali kwa ajili ya kupitia mikataba ya madini, gesi na mafuta ni moja ya makubaliano katika utekelezaji wa Dira ya Madini ya Africa (Mining Vision for Africa) iliyoasisiwa na wakuu wa nchi zenye madini katika mkutano wake uliofanyika mwaka 2009. 
 Alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inachangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika zinazozalisha madini wakuu wa nchi walikubaliana kuanzishwa kwa Dira ya Madini itakayowezesha sekta ya madini katika nchi wanachama kuboreshwa na kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi 
Alisema kuwa katika utekelezaji wa Dira ya Madini ya Afrika, nchi ya Tanzania imeanza kutoa mafunzo kwa wataalam mbalimbali katika taasisi za Serikali katika upitiaji wa mikataba hususan ya utafiti na uchimbaji wa rasilimali za madini, gesi na mafuta. Alisisitiza kuwa mara baada ya wataalam hao kupata mafunzo wataweza kupitia mikataba mbalimbali kabla ya kusainiwa. 
“Ieleweke kwamba suala la mikataba litakuwa si kati ya watu wawili bali wataalam watashirikishwa kwa kupitia mikataba hiyo na kutoa mapendekezo yao kabla ya mikataba kusainiwa na Waziri ambaye ni msimamizi wa sekta husika,” alisisitiza Simbachawene. Akielezea ushirikishwaji wa wananchi katika usimamizi wa sekta za madini, gesi na mafuta, Simbachawene alisema kuwa Serikali imehakikisha kuwa mikataba yote inalenga kuwanufaisha wananchi kwa kushirikishwa katika utoaji wa huduma katika sekta husika. 
Akitolea mfano wa sekta ya gesi nchini, alisema fursa za utoaji wa huduma zipo nyingi na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hizo Hata hiyo alieleza kuwa Serikali ina mkakati wa kutoa mafunzo kwa wanachi kuhusu uzalishaji wa bidhaa bora ili ziendane na soko la kimataifa. 
“ Tunataka ifike mahali makampuni yanayofanya shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini, gesi na mafuta yanunue huduma na bidhaa kwa wananchi wa Tanzania badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi,” alisisitza Simbachawene. 
Naye mtaalam kutoka Kitengo cha Nishati na Mabadiliko ya Tabia Nchi, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Abbas Kitogo alisema kuwa shirika la UNDP limekuwa likishirikiana na Serikali katika utoaji wa mafunzo kuhusu sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na usimamizi wa mikataba 
Alisema sekta nyeti kama za madini, gesi na mafuta zisiposimamiwa kikamilifu zinaweza kuibua migogoro badala ya kuleta maendeleo. 
 
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia) akifungua  warsha kuhusu Dira ya Madini Afrika  iliyokutanisha wataalam kutoka   taasisi za serikali nchini lengo likiwa ni kuwapa uelewa juu  ya sekta ya madini na usimamizi wa mikataba. Katikati ni Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu na Mbadala Mhandisi Edward Ishengoma. Kushoto ni mtaalam kutoka  Kitengo cha  Nishati na Mabadiliko ya Tabia Nchi, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Abbas Kitogo.
 Washiriki  wa warsha kuhusu Dira ya Madini Afrika wakifuatilia kwa makini  hotuba ya ufunguzi iliyokuwa inatolewa na Waziri wa Nishati na Madini, George  Simbachawene (hayupo pichani)
Picha ya pamoja baada ya ufunguzi

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...